info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

“TTCL NI MHIMILI MUHIMU KUELEKEA TANZANIA YA KIDIJITALI" – PROFESA SHEMDOE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe Profesa Riziki Shemdoe ametoa rai kwa wananchi kutumia huduma zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) huku akipongeza juhudi za Shirika hilo katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga Tanzania ya kidijitali na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano.

Profesa Shemdoe ameyasema hayo alipotembelea banda la TTCL katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. Maonesho hayo yalianza Juni 16 na kuhitimishwa Juni 23, 2026, yakiwa na kaulimbiu isemayo, "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu."

Akiwa katika banda la TTCL, Profesa Shemdoe alipata fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo huduma za mawasiliano ya simu, intaneti pamoja na huduma za TEHAMA zinazolenga kuharakisha utekelezaji wa Serikali ya Kidijitali.

Amesema TTCL imeendelea kuwa mhimili muhimu katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini kwa kuhakikisha huduma zake zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, jambo linalochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"TTCL ni shirika la kimkakati ambalo limekuwa likitoa huduma za mawasiliano kwa lengo la kurahisisha mawasiliano kwa kila Mtanzania. Ni muhimu wananchi kuendelea kutumia huduma zake na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa kidijitali," amesema Profesa Shemdoe.

Ushiriki wa TTCL katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma umeiwezesha jamii kupata uelewa mpana zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo pamoja na nafasi yake katika kufanikisha dira ya Tanzania ya uchumi wa kidijitali.