TTCL NGUZO MUHIMU YA TEKNOLOJIA KATIKA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI NA UCHUMI WA KIDIJITALI
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kujidhihirisha kama mdau mkuu wa teknolojia nchini kwa kusisitiza umuhimu wa miundombinu ya intaneti na mawasiliano ya kisasa katika kufanikisha utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na kukuza uchumi wa kidijitali.
Hatua hiyo imebainishwa wakati wa Kongamano la Mwaka la Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Huduma za Posta linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Mauzo wa TTCL, Bi. Linda Mushi, alisema kuwa TTCL inaendelea kuwekeza na kupanua huduma za intaneti na teknolojia za mawasiliano kwa kushirikiana na Shirika la Posta Tanzania pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kuhakikisha mifumo ya kidijitali inawafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa TTCL, kama mtoa huduma wa Kitaifa wa mawasiliano, ina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za intaneti unakuwa chachu ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi, unaotarajiwa kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, biashara na utawala.
Bi. Mushi alieleza kuwa kupitia miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, TTCL inaunga mkono juhudi za serikali katika kujenga uchumi wa kidijitali kwa kuwezesha matumizi ya huduma za posta za kidijitali, mifumo ya anwani mahiri na ubunifu wa teknolojia unaolenga ukuaji jumuishi.
Kongamano la mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu isemayo “Anwani Mahiri na Ubunifu wa Huduma za Posta kwa Ukuaji Jumuishi”, kauli mbiu inayosisitiza nafasi ya teknolojia katika kuboresha huduma za posta na kuhakikisha zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi.
Ushiriki wa TTCL katika kongamano hilo unaonesha dhamira ya shirika hilo katika kuendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano nchini, hususan katika kuimarisha mifumo ya kidijitali inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.