info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL NA YAS BUSINESS WAIMARISHA USHIRIKIANO UTEKELEZAJI WA AGENDA YA TANZANIA YA KIDIJITALI

Katika jitihada za kukuza uchumi wa kidijitali na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini, Shirika la Mawasiliano kwa kushirikiana na Kampuni ya YAS Business wamefanya KikaoKkazi cha Kimkakati, kilicholenga kuendeleza ushirikiano na kuchochea jitihada za mageuzi ya ujenzi wa Tanzania ya kidigitali kupitia miundombinu bora za mawasiliano.

Kwa zaidi ya muongo mmoja, TTCL na YAS Business wamekuwa washirika wa karibu katika sekta ya mawasiliano hapa nchini huku ushirikiano huo ukichochea ufanisi wa kasi kutokana na ubadilishanaji wa utaalamu wa kitaalamu, uboreshaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi katika matumizi ya miundombinu ya TEHAMA kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kikao hicho muhimu kimewakutanisha wataalamu wa Ufundi na Biashara kutoka TTCL na YAS, kikilenga kufanikisha mwelekeo wa pamoja wa kimkakati kwa maendeleo ya TEHAMA, kuchambua na kutathmini fursa mpya za biashara ndani na nje ya Tanzania.

Pia kililenga kujadili njia bora za matumizi ya pamoja ya miundombinu ya Mkongo wa Taifa, kuweka msingi thabiti wa ushirikiano wa miundombinu ya mawasiliano na kusaidia ajenda ya Taifa ya mageuzi ya kidijitali.

Kupitia majadiliano ya kikao hicho, pande zote mbili zimeonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kushirikiana katika kukuza na kuimarisha mtandao wa mawasiliano ya kisasa hapa nchini.

Katika hatua nyingine muhimu za kukuza miundombinu ya mawasiliano, TTCL hivi karibuni imezindua rasmi maunganisho kati ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na mikongo ya baharini ya kimataifa iliyopo Mombasa, Kenya. 

Maunganisho hayo yanalenga kuimarisha kasi, ubora na upatikanaji wa huduma za intaneti ndani ya nchi na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki huku matarajio yakiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa upitishaji wa data kwa kasi ya juu, kuboresha ubora wa huduma kwa wateja wa ndani na wa kimataifa, kuchochea maendeleo ya sekta ya TEHAMA na uchumi wa kidijitali nchini na kuwezesha fursa mpya za uwekezaji na ubunifu.

Ushirikiano kati ya TTCL na YAS Business unaendelea kuwa mfano wa mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta ya Umma na Binafsi katika kutekeleza agenga ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta mapinduzi ya kidijitali na matumizi ya TEHAMA nchini.