info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL NA BBS YA BURUNDI WAENDELEA KUBORESHA MAHUSIANO YA KIBIASHARA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), na Burundi Backbone System (BBS) wamesaini mkataba wa kuongeza uwezo wa huduma za mawasiliano nchini Burundi kutoka 4Gbps hadi 10Gbps.

Mkataba huo umesainiwa leo, Septemba 8, 2026, katika Ofisi za Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa BBS, Bw. Diegue Nifasha, pamoja na ujumbe wake kutoka Burundi, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Alex Biziriko, akiongozana na wataalamu kutoka idara na vitengo mbalimbali vya TTCL.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Biziriko amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya TTCL na BBS, sambamba na kuongeza uwezo wa nchi hizo mbili kupata huduma za mawasiliano zenye uwezo mkubwa, salama na za kuaminika.

Amesema TTCL, kupitia NICTBB, imeendelea kuihudumia Burundi kwa huduma za muunganisho wa kimataifa kupitia BBS, huku makubaliano mapya yakilenga kuongeza uwezo wa mawasiliano kutoka 4Gbps hadi 10Gbps.

Kwa mujibu wa Bw. Biziriko, ongezeko hilo linatokana na kuendelea kukua kwa mahitaji ya huduma za kidijitali nchini Burundi, hususan huduma zinazohitaji uwezo mkubwa, uhakika na usalama wa mawasiliano.

Aidha, ameipongeza BBS pamoja na Serikali ya Burundi kwa kuendelea kushirikiana na TTCL katika kuendeleza miundombinu na huduma za muunganisho wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bw. Biziriko amesema NICTBB inaendelea kuwa kichocheo muhimu cha mageuzi ya kidijitali kwa kuwezesha huduma katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, huduma za Serikali, elimu na afya, pamoja na maeneo mengine ya kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa makubaliano hayo hayaishii katika kuongeza uwezo wa mawasiliano pekee, bali pia yanaimarisha kiungo cha kidijitali kati ya Tanzania na Burundi na kuchangia juhudi za kupanua muunganisho wa kikanda na kukuza uchumi wa kidijitali.

“Makubaliano ya leo yanawakilisha zaidi ya ongezeko la uwezo wa mawasiliano. Yanaimarisha kiungo cha kidijitali kati ya Tanzania na Burundi, yanaongeza ushirikiano wetu na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali,” amesema Bw. Biziriko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa BBS, Bw. Diegue Nifasha, amesema Burundi inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali na kwamba ongezeko la uwezo wa mawasiliano hadi 10Gbps ni sehemu muhimu ya mabadiliko hayo.

Amesema mahitaji ya huduma za mawasiliano nchini Burundi yanaendelea kukua kwa kasi, hali inayoweza kusababisha hitaji la kuongeza uwezo huo zaidi hata kabla ya kumalizika kwa kipindi cha miaka miwili kilichowekwa katika mkataba.

“Nchi yetu inaelekea kwenye uchumi wa kidijitali, na ninaamini huu ni mwanzo tu. Mahitaji yataendelea kukua kwa kasi kubwa, hivyo ongezeko hili la kufikia 10Gbps ni hatua muhimu inayofuata,” amesema Bw. Nifasha.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya BBS na TTCL hautajikita katika kuongeza uwezo wa mawasiliano pekee, bali unatarajiwa kupanuka katika maeneo mengine ya kiutendaji, ikiwemo kubadilishana uzoefu, maarifa na kujenga uwezo wa wataalamu kutoka pande zote mbili.

Amesema BBS ipo tayari kutuma wataalamu wake kujifunza na kubadilishana uzoefu na wenzao wa TTCL, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati baina ya taasisi hizo mbili.

Bw. Nifasha ameeleza matumaini kuwa mkataba huo ni mwanzo wa ushirikiano mpana zaidi kati ya BBS na TTCL katika maeneo mbalimbali ya teknolojia na mawasiliano, kwa manufaa ya Tanzania na Burundi.

Kusainiwa kwa mkataba huo kutaimarisha zaidi muunganisho wa mawasiliano kati ya Tanzania na Burundi, kukidhi ongezeko la mahitaji ya huduma za kidijitali na kufungua fursa mpya za ushirikiano katika sekta ya TEHAMA. Hatua hiyo pia inaendelea kuimarisha nafasi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kama kiungo muhimu cha mawasiliano ya kikanda na kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa kidijitali katika nchi za Afrika Mashariki.