
TTCL KUJENGA MINARA ZAIDI YA 1,400 KUIMARISHA MAWASILIANO NCHINI
Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Bw. Moremi Marwa, amesema katika Mwaka wa Fedha 2025/2026 Serikali kupitia shirika hilo limepanga kujenga zaidi ya minara 1,400 ya mawasiliano nchini, ikianza na minara 626 mwaka huu, na mingine 850 kufuata mwaka 2026/2027.
Bw. Marwa ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Jijini Arusha katika banda la TTCL kwenye Kikao Kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC – Arusha.
Amesema TTCL ndiyo shirika pekee nchini linalomiliki Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, huku Serikali ikiendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa ili kufanikisha ajenda ya uchumi wa kidijitali.
“Hatua hii inalenga kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na yenye changamoto ambazo kwa kawaida watoa huduma binafsi hawawezi kufika kutokana na maeneo hayo kutokuwa na mvuto wa kibiashara,” amesema Marwa.
Aidha, amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu miezi sita iliyopita, zaidi ya minara 100 imekwishajengwa, na matarajio ni kwamba ifikapo Juni 2026, minara yote 626 iliyopangwa kwa mwaka huu itakuwa imekamilika.
Ameongeza kuwa TTCL imejipanga kuhakikisha minara hiyo inaunganishwa moja kwa moja na Mkongo wa Taifa ili wananchi wapate huduma za intaneti yenye kasi na uhakika.
Aidha amekumbusha kuwa mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mkakati wa kidijitali unaolenga kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka msisitizo mkubwa katika eneo hilo.
Mbali na Mkongo wa Taifa, TTCL pia ina kituo cha Data Center kinachowezesha mifumo ya kidijitali nchini kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Uwekezaji huu unaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya teknolojia, huku wananchi wakinufaika na huduma bora za mawasiliano, ikiwemo intaneti ya kasi kubwa inayosaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Bw. Moremi Marwa, ameungana na viongozi wengine wa mashirika ya umma kushiriki kikao hiki kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Philip Mpango, na kimebeba kaulimbiu muhimu inayosema: “Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara katika Mazingira Shindani ya Kimataifa – Nafasi ya Mashirika ya Umma.”