info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL KUJENGA MINARA 636 KUIMARISHA MAWASILIANO NCHINI

SERIKALI kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linatarajia kujenga minara 636 Tanzania nzima katika maeneo ya pembezoni ya miji ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchi nzima. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi alipotembelea Ofisi za TTCL Makao Makuu Oktoba 12, mwaka huu katika ziara yake ya kikazi kutembelea Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara anayoisimamia. 

Alisema kuwa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kusainiwa kwa mkataba kujenga minara 636 nchi nzima kwa ajili ya kupeleka huduma kwa wananchi ili kuchochea shughuli za maendeleo. 

Mkataba huo uliosainiwa Septemba mwaka huu unalenga kutekelezwa katika maeneo ambayo bado huduma ya mawasiliano haijafika vizuri na matarajio ya serikali ni kuwa wasimamizi wa kazi hiyo wataifanya kwa uhakika ili wananchi wanaoishi pembezoni mwa mji wanapata huduma bora za mawasiliano.

"Tunaamini kwa maelekezo ambayo tumepeana watakwenda kusimamia kazi hii lengo ni kuona mwananchi wa Tanzania yule ambaye yupo pembezoni mwa mji anaweze kufikiwa na huduma za mawasiliano.

Awali serikali ilisaini mkataba na watoa huduma za mawasiliano nchini kutekeleza ujenzi wa minara 757, katika utekelezaji huo TTCL ilipewa minara 200 ambapo utekelezaji unaendelea ikiwa minara michache tayari inafamnya kazi na mingine inaendelea katika hatua ya utekelezaji huku lengo la serikali ni kuona maeneo ambayo yako pembezoni mwa miji yaweze kuboreshwa kimawasiliano.

Katika ziara hiyo iliyolenga kujadili maendeleo ya TEHAMA nchini, Mhe. Mahundi alipokelewa na Mwenyeji wake ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo CPA Moremi Marwa ambapo pamoja na mambo mengine alielezwa kwa kina kuhusu hatua mbalimbali ambazo TTCL imechukua katika kuboresha miundombinu yake ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika na ya kisasa kwa Wananchi.

Mkurugenzi Mkuu, CPA. Moremi Marwa alimweleza Mhe. Naibu Waziri jinsi Shirika hilo linavyojikita katika kuhakikisha miradi ya mawasiliano ikiwemo miradi ya ujenzi wa minara inakamilika kwa wakati ili kufanikisha adhima ya Serikali ya kufikisha huduma za mawasiliano maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya vijijini.

Wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea vituo vya kiufundi vya TTCL, kuzungumza na Watumishi wa shirika hilo na kuona uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo Mahili cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC). 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mahundi aliipongeza Menejimenti ya TTCL kwa jitihada zake katika kusimamia na kuendesha miundombinu ya mawasiliano na kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha wananchi hao kufaidika na fursa zinazotokana na teknolojia ya mawasiliano.

Katika hatua nyingine Mhe. Mahundi alisema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umekuwa kivutio barani Afrika baada ya Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania kufanikisha kuunganisha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika -SADC 

“Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umekuwa kivutio kikubwa kwani mpaka sasa tumeweza kutoa huduma katika nchi sita ikiwa ni pamoja na Kenya, Malawi, Burundi, Zambia Uganda, Rwanda, hawa wote wanaweza kupata mawasiliano kwenye nchi zao kwa kutegemea Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao Mhe. Rais aliruhusu fedha nyingi kutumika” alisema Mhe. Mahundi.

Aidha, Mhe. Mahundi amepongeza wataalamu wa ndani wa shirika hilo kwa kujenga Mkongo wa Taifa na utekelezaji wa mikakati ya upanuzi wa Mkongo ili kuleta tija kwa Taifa. 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa amezikaribisha kampuni za mawasiliano, sekta binafsi na sekta za umma nchini kutuimia Data Center kuhifadhi data zao katika kituo hicho kwa ajili ya usalama wa data za kampuni zao.

Aidha aliishukuru Serikali kwa kuiwezesha TTCL ili wawafikie wananchi wote nchini kwa kuwapa huduma za mawasiliano ili kuendana na kasi ya maendeleo na teknolojia.

Ziara ya Mhe. Mahundi ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inabaki kuwa nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. TTCL, kama shirika la umma, limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia juhudi za Serikali za kupanua wigo wa mawasiliano nchini kote.