TTCL KITOVU CHA MAENDELEO SEKTA YA MAWASILIANO
Imeelezwa kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ni kitovu cha maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano na kitovu cha maendeleo ya uchumi wa Kidigitali nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mhandisi Peter Ulanga alipokuwa akizungumza wakati wa mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliolenga kuelezea mafanikio na malengo ya Shirika hilo, Mhandisi Ulanga amewambia Wahariri hao kuwa TTCL inatimiza majukumu yake katika sura mbili, moja ikiwa ni kuwahudumia wateja wakawaida na jukumu la pili ni kuwa chombo wezeshi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Amesema katika eneo la miundombinu wezeshi ya mawasiliano Shirika linalo jukumu kubwa la kuhakikisha huduma inapatikana muda wote kwani kwa mazingira yoyote ya kukosekana kwa huduma ya mawasiliano kunaathiri watoa huduma wengine wa mawasiliano.
"Kama ikitokea kwa sababu yoyote mawasiliano ya Shirika yakasimama kufanya kazi hakuna huduma ya Mawasiliano itakayoweza kuendelea sababu wateka wetu wakubwa ni Vodacom, Airtel, Tigo, Halotel, Serikali kuu na nchi Jirani kama Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia nk" amesema Mhandisi Ulanga.
Aidha amesema TTCL inalo jukumu la kusimamia na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na sasa kupitia miundombinu hiyo TTCL inatoa huduma ya Faiba Mlangoni ambayo inampatia mteja intaneti kwa viwango vya juu vya ubora.
Mhandisi Ulanga amesema faiba mlangoni imeleta mapindizi ya matumizi ya intaneti nyumbani na katika ofisi mbalimbali kwani huduma hiyo ni ya gharama nafuu zaidi.
Amesema Shirika hilo linayo matarajio ya kuziunganisha Wilaya mia moja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ifikapo Januari 2024 na kwamba zitakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi kwa ufanisi wa hali juu.
Amewataka wananchi kutambua kuwa wanapoona maendeleo katika sekta ya mawasiliano waelewe kuwa TTCL ndiyo kinara wa uwezeshaji wa maendeleo hao.