info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL CHACHU YA MAPINDUZI YA KIDIJITALI KATIKA SOKA ZANZIBAR

Na Adeline Berchimance

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema ushirikiano kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) una fursa kubwa ya kubadilisha uendeshaji wa soka Zanzibar kwa kutumia teknolojia za kidijitali.

Dkt. Pembe amesema ushirikiano huo unapaswa kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za mawasiliano na kwenda kwenye kutumia teknolojia kama nyenzo ya kufungua fursa za kiuchumi, kuongeza ushiriki wa wananchi na kuunganisha wadau mbalimbali wa soka.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ushirikiano kati ya TTCL na ZFF Waziri Pembe amesema majukwaa ya kidijitali yanaweza kutumika katika maeneo mbalimbali ya michezo, yakiwemo matangazo, mauzo ya bidhaa za michezo, huduma kwa washiriki, mahusiano na mashabiki, biashara ya bidhaa za timu na udhamini.

“Majukwaa haya yanaweza kutumika kama matangazo, mauzo ya michezo, mahusiano, huduma kwa washiriki, biashara ya bidhaa za timu, udhamini na maeneo mengine,” amesema Dkt. Pembe.

Amesema matumizi hayo yanaweza kuongeza thamani ya soka Zanzibar kwa kuwafikia watu wengi zaidi na kuwapa wadau fursa pana za kushiriki katika shughuli za michezo, huku yakichangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Dkt. Pembe amesema Wizara ya Habari pamoja na Wizara inayohusika na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar zina nafasi muhimu katika kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanawafikia wananchi wengi zaidi na kuleta matokeo katika sekta ya michezo.

Amesema hatua ya TTCL na ZFF kuingia katika ushirikiano huo ni muhimu katika kutekeleza mikakati ya maendeleo ya soka Zanzibar, huku akiwataka wadau kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na teknolojia.

Amesema kupitia teknolojia, taarifa na fursa zinazohusiana na michezo zinaweza kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi, huku wadau wakiwa na nafasi ya kutumia majukwaa hayo katika kukuza biashara na shughuli zao.

Dkt. Pembe amesema Serikali itaendelea kushirikiana na TTCL, ZFF na wadau wengine katika kuhakikisha malengo ya ushirikiano huo yanatekelezwa na kuleta matokeo yanayoonekana na kuongeza kuwa mafanikio ya mpango huo yanahitaji ushirikiano wa viongozi, taasisi, wanamichezo, vyombo vya habari, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Tunapaswa kutembea pamoja ili kufikisha jambo hili mbali zaidi,” amesema, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano katika kuendeleza michezo na Taifa.