TANZANIA YANG’ARA KUPITIA TTCL — WBBA YAITAMBUA KAMA KINARA WA MIUNDOMBINU YA KIDIJITALI AFRIKA
Tanzania imeendelea kung’ara katika ramani ya maendeleo ya TEHAMA barani Afrika baada ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kutunukiwa tuzo ya heshima ya “Gigacity Champion” na World Broadband Association (WBBA) katika mkutano wa WBBA Africa Summit South, uliofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini.
Mkutano huo wa Kimataifa, uliofanyika sambamba na Africa Tech Festival, ni jukwaa la juu linalowakutanisha Viongozi wa serikali, Wataalamu wa teknolojia, Watoa Huduma za Mawasiliano, na wadau wa sekta ya broadband kutoka barani Afrika na Duniani.
Lengo kuu la mkutano huo uliofanyika Novemba 10 mwaka huu ilikuwa ni kuchochea kasi ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya broadband na kuhimiza ushirikiano wa kimkakati katika mageuzi ya kidijitali barani Afrika.
Akizungumza katika kikao maalum cha Broadband Development Conference (BDC), Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, aliwasilisha mada yenye kichwa cha habari “Establish a Fiber Foundation to Pave the Future for Tanzania”, akieleza hatua kubwa zilizofikiwa na Tanzania kupitia mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ambao umeweka msingi imara wa uchumi wa kidijitali nchini.
Kupitia hotuba hiyo, Bw. Marwa alibainisha kuwa TTCL imejikita katika kupanua mtandao wa nyaya za optic fiber ili kufikia maelfu ya kilomita na kuunganisha Mikoa yote ya Tanzania pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, na Msumbiji, uwekezaji ambao umeifanya Tanzania kuwa kiungo muhimu cha mawasiliano kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Kwa kutambua mchango huo, Mkurugenzi Mkuu wa WBBA, Martin Creaner, alikabidhi rasmi tuzo kwa TTCL akisema: “TTCL imeonesha uongozi na dira ya kipekee katika kuandaa miundombinu ya broadband yenye uwezo wa Gigabit, inayowezesha ujenzi wa miji mahiri na uchumi wa kidijitali unaoendeshwa na maarifa.”
Tuzo ya “Gigacity Champion” inatambua mafanikio ya TTCL katika kusimamia mradi wa NICTBB, kupanua mtandao wa Kitaifa na wa Kikanda, na kuwezesha huduma za kisasa kama Serikali mtandao, Afya mtandao, Elimu mtandao, Kilimo mtandao pamoja na uchumi wa kidigitali. Aidha TTCL pia imekuwa chachu ya ubunifu wa miji mahiri, mageuzi ya kiuchumi, na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika kwa wananchi.
Kupitia mafanikio haya, Tanzania imethibitisha dhamira ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2025, ambayo inalenga kuifanya nchi kuwa uchumi wa kati unaoendeshwa na teknolojia, ubunifu, na maarifa, huku TTCL ikiendelea ikiendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya broadband, ikiwemo upanuzi wa Mkongo wa Taifa hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Ziwa Tanganyika, pamoja na miradi ya miji mahiri, viwanda vya vifaa vya kidigitali na upanuzi wa huduma za Wi-Fi bure katika maeneo ya Umma.
Kwa kutunukiwa heshima hii ya kimataifa, TTCL imeweka rekodi mpya kama nguzo kuu ya mageuzi ya kidijitali Afrika, ikithibitisha uwezo wa Tanzania kuwa kitovu cha TEHAMA na mawasiliano barani Afrika.