info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TANZANIA NA KENYA WAZINDUA MAUNGANISHO YA MKONGO WA MAWASILIANO

Tanzania na Kenya zimeandika historia mpya katika ushirikiano wa kidijitali baada ya kuzinduliwa rasmi kwa miundombinu ya kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Tanzania kupitia Kituo cha Horohoro hadi ICOL Data Center, Mombasa, Kenya.

Tukio hili muhimu limefanyika Julai 18, mwaka huu na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa sekta ya mawasiliano kutoka nchi zote mbili pamoja na wadau wa mbalimbali.

Hatua hii ya kihistoria inalenga kuimarisha ushindani wa kidijitali, kupanua wigo wa huduma za mawasiliano ya kasi kubwa, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa dijitali siyo tu kwa Tanzania na Kenya, bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Kuunganishwa kwa Mkongo wa Taifa na ICOL Data Center ni hatua kubwa katika juhudi za Tanzania na Kenya kuhakikisha zinatoa huduma bora, thabiti na nafuu za mawasiliano kwa wananchi na wafanyabiashara na itafungua milango kwa Mataifa haya kuwa kitovu cha kidijitali kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mhe. Jerry Silaa na waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidigitali wa Kenya, Injinia William Kabogo Gitau, pamoja na 

Mawaziri hao wamesisitiza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria, ikilenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya uhakika, pamoja na kupunguza changamoto za kukatika kwa mtandao.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo Mhe. Jerry Silaa alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya pamoja ya mawasiliano kati ya nchi washirika ni wajibu wa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya kikanda.

“Kuna faida kubwa ya kuwa na maunganisho mengi ya mikongo ya mawasiliano. Hii husaidia kuwepo kwa mtandao wa uhakika, unaotegemewa hata wakati wa changamoto za kiufundi katika njia moja ya mawasiliano,” alisema Silaa.

Naye Waziri Gitau amesema: “Jambo la msingi ni ushirikiano wa dhati kati ya nchi zetu mbili. Ni muhimu kuhakikisha tunatunza miundombinu hii ya kimkakati ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababisha kukatika kwa umeme na mtandao. Pia tuendelee kuimarisha mahusiano yetu kwa manufaa ya pande zote.”

Mradi huu ni sehemu ya juhudi pana za kuunganisha Afrika kupitia Mkongo wa Taifa unaomilikiwa na Serikali ya Tanzania chini ya TTCL, ambao tayari umeunganishwa na nchi za Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na Uganda. Kwa sasa, Tanzania inajidhihirisha kuwa kiungo muhimu katika mawasiliano kikanda, ikiweka msingi wa uchumi wa kisasa unaotegemea TEHAMA.

Kuzinduliwa kwa mradi huu kumeweka msingi thabiti wa ushirikiano wa kimkakati wa kidijitali kati ya Tanzania na Kenya, huku matarajio yakiwa ni kuona ongezeko la huduma za kisasa na maendeleo ya teknolojia yanayowanufaisha mamilioni ya wananchi katika Afrika Mashariki.