info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TANZANIA NA DRC KUUNGANISHWA KUPITIA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia Kikao cha kimkakati na Shirika la Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SOCOF) kuhusu mpango wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) kutoka Kigoma, kupitia Ziwa Tanganyika, hadi kufikia jimbo la Kalemie nchini DRC.

Kikao hicho maalum kimefanyika Makao Makuu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) jijini Dar es Salaam kikiwakutanisha Wataalam wa TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa SOCOF, Bw. Prosper Ghislain.

Kikao hicho kimejadili mpango wa kupanuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma, kupitia Ziwa Tanganyika, hadi kufikia jimbo la Kalemie nchini DRC hatua inayolenga kuimarisha mawasiliano na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa pande zote mbili.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, amesema shirika linaendelea kujivunia nafasi yake ya kuwa kiunganishi muhimu cha miundombinu ya mawasiliano katika kanda.

“Tanzania imeendelea kusimama kama kitovu cha mawasiliano ndani ya EAC na SADC, ikichochea ukuaji wa teknolojia na miundombinu kupitia NICTBB,” alisema Bw. Marwa, akisisitiza kuwa miradi kama hii ni nguzo ya maendeleo ya uchumi wa kidigitali.

Kwa upande wake, Bw. Prosper Ghislain, Mkurugenzi Mkuu wa SOCOF, amesema muunganiko wa Mkongo wa Mawasiliano kati ya Tanzania na DRC utarahisisha mawasiliano, kuongeza ufanisi wa huduma za kidigitali na kuchochea biashara katika ukanda huo. 

“Tunaiona Tanzania kama kiungo muhimu cha kuunganisha nchi za Kaskazini na Kusini mwa Afrika,” amesema Ghislain.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba aamesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuonesha uimara wa Tanzania kama kitovu cha mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kusini, na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia huduma za mawasiliano zenye kasi, uhakika na ubunifu.