info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

T-PESA YAUNGANISHA NGUVU YA WANAWAKE NA FURSA ZA UCHUMI WA KIDIJITALI

Na Debora Ngalima

Mwanamke anapowezeshwa kuongoza na kujitegemea kiuchumi, anafungua milango ya fursa si kwake pekee, bali pia kwa familia, jamii na taifa. Nguvu hiyo inapounganishwa na maarifa ya kifedha na teknolojia, inakuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, T-PESA imedhamini mkutano wa wanawake viongozi uliofanyika Novemba 19, 2026, katika Hoteli ya Urban by CityBlue, Masaki, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha uongozi, uwekezaji na ushiriki wa wanawake katika uchumi wa kidijitali.

Mkutano huo, uliopewa jina la “Women Leading with Purpose”, umeandaliwa na Women Leadership in Insurance Africa kwa kushirikiana na GIG Consult, chini ya kaulimbiu ya “Kuongoza kwa Dira, Kuhamasisha Mabadiliko”, ukilenga kuwajengea wanawake uwezo wa kuongoza kwa maono, kujiamini na kufanya maamuzi ya kimkakati.

Kupitia udhamini huo, T-PESA imeonyesha dhamira ya kuunga mkono uwezeshaji wa wanawake kwa kuwaunganisha na maarifa, fursa za kifedha na teknolojia zinazoweza kuchochea maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Mkutano huo umejikita katika mijadala kuhusu uongozi bora, uthubutu wa kutafuta fursa, kujenga timu zenye mafanikio na kufanya maamuzi sahihi. Aidha, washiriki wamejadili umuhimu wa usimamizi wa fedha, uwekezaji na kujenga misingi imara ya kujitegemea kiuchumi.

Masuala hayo yanaendana na nafasi ya T-PESA katika sekta ya huduma za fedha za kidijitali, inayochangia kurahisisha miamala, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kupanua fursa za biashara na ujasiriamali.

Mbali na uongozi na uchumi, mkutano huo umeangazia afya na ustawi wa wanawake kupitia majadiliano yaliyoongozwa na Dkt. Matilda Ngarina, yakisisitiza umuhimu wa afya katika kufanikisha malengo binafsi na ya kiuongozi.

Udhamini huo pia umefungua fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta za bima, fedha na teknolojia katika kuongeza ujumuishaji wa kifedha, hususan kwa wanawake na wajasiriamali.

Kwa T-PESA, kudhamini mkutano huu ni zaidi ya kuunga mkono tukio la siku moja; ni sehemu ya kuchangia katika kujenga jamii ya wanawake wenye maarifa, ujasiri na uwezo wa kutumia fursa za uchumi wa kidijitali.

Hatua hiyo inasisitiza kuwa mustakabali wa uchumi wa kidijitali haujengwi na teknolojia pekee, bali pia na wanawake wenye uwezo wa kuitumia kuleta maendeleo endelevu kwa jamii na taifa.