T-PESA YASHIRIKI KIKAMILIFU UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA WIKI YA HUDUMA ZA FEDHA KITAIFA
Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), T-PESA, imeshiriki kikamilifu katika ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha za kidijitali, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu ujumuishaji wa kifedha, pamoja na kuhimiza ushiriki wa wadau mbalimbali katika kukuza sekta ya huduma za fedha nchini.
Ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo umefanywa na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), ambaye amesisitiza umuhimu wa huduma za fedha za kidijitali katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wote.
Mhe. Luswetula ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia katika huduma za fedha yamekuwa chachu ya ujumuishaji wa kifedha, hasa kwa wananchi walioko maeneo ya vijijini na pembezoni, na hivyo kusaidia kukuza uchumi jumuishi na endelevu.
Katika hafla hiyo ya ufunguzi, Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea Banda la Maonesho la T-PESA, ambapo watoa huduma walimweleza huduma mbalimbali za kifedha za kidijitali zinazotolewa na kampuni hiyo, zikiwemo huduma za malipo, uhamishaji wa fedha pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Kupitia maonesho hayo, T-PESA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia huduma za fedha kupitia Kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya mifumo salama, urahisi na unafuu wa gharama na jinsi inavyochangia ustawi wa jamii.
Katika hafla ya ufunguzi Kaimu Meneja Mkuu T-PESA, Bi. Mariana Batibo, alisisitiza utayari wa kampuni hiyo kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuboresha, kupanua na kuimarisha huduma za fedha za kidijitali nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.