T-PESA YAPONGEZWA UTOAJI HUDUMA
Watumishi wa Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania, T-PESA wamepongezwa kwa utoaji bora wa huduma ya fedha kimtandao nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo Bw. Richard Mayongela, alipokuwa akizungumza mbele ya Wajumbe wa Bodi ya T-PESA wakati akihitimisha Kikao cha siku mbili cha Mapitio ya Kimkakati ya T-PESA kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Maasai (Ledger Plaza) uliopo Bahari Bichi, Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 11 hadi 12 mwaka huu.
Bw. Mayongela kwa namna ya pekee aliupongeza uongozi wa T-PESA kwa namna ambavyo umekuwa ukitekeleza majukumu yake na kuendesha shughuli za utoaji wa huduma za fedha kupitia Simu za Mkononi.
Alisema kwa juhudi hizo zilizofanyika ni wazi kuwa kupitia majadiliano yaliyofanyika katika Kikao hicho cha Mapitio ya Kimkakati ya T-PESA kutoka kwa wataalam wa masuala ya huduma za kifedha kielektroniki yataonesha ramani na njia nzuri ya kufikia mipango na malengo yaliyowekwa na Kampuni katika kuwahudumia wananchi.
“Kitu kizuri zaidi tumepata watu ambao wanauzoefu wa kutosha katika utoaji wa huduma za Kifedha Kielektroni kupitia Simu za Mkononi na wametupitisha katika hatua mbalimbali za Kimkakati kwa vitendo. Hii itatusaidia katika kutimiza Mikakati na Malengo tuliyoweka na Kampuni” Alisema Mayongela.
Katika hatua nyingine Bw. Mayongela alisema kuwa Kampuni ya T-PESA inatakiwa kujipanga na kuwa tayari kukabiliana na mabadiliko ya aina yoyote hasa ya Kiteknolojia yanayoweza kujitokeza na kuigusa Kampuni kwa namna moja ama nyingine
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa T-PESA, Bi Lulu Mkudde alisema T-PESA imekuwa katika mpango wa kuweka sawa Mikakati iliyonayo ikiwa ni pamoja na kujua mwenendo wa Masoko na ukuwaji wa Teknolojia ili kuhahakisha Kampuni hiyo inaendelea kutoa huduma bora za kifedha kupitia Simu za Mkononi na kufikia lengo walilojiwekea la kuifanya T-PESA kuwa lango la Malipo ya Kidijitali hapa nchini.
Bi. Mkudde alisema katika kipindi cha miaka michache iliyopita T-PESA ilikumbana na changamoto hivyo kupitia Mapitio ya Kimkakati yaliyofanyika ni Imani yao kuwa yatatoa njia sahihi kuelekea katika Mafanikio na kutimiza Malengo yaliyowekwa.
Wawasilishaji wakuu katika Kikao hicho cha Mapitio ya Kimkakati ya Kampuni ya T-PESA, ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Red anti International ya nchini Kenya, Bi. Catheline Kichunge pamoja na Bi. Abigal Komu kutoka red anti International ambaye ni mbobezi wa maswala ya fedha Kidijitali (Digital finance).
Mpaka kufikia sasa T-PESA imewafikia wateja mbalimbali nchi nzima kupitia huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kufanya miamala ya kutuma na kupokea fedha, kulipa bili mbalimbali ikiwemo bili za maji, umeme, ving’amuzi Pamoja na malipo mbalimbali za Serikali.