T-PESA YAIBUKA MSHINDI WA TATU KATIKA WIKI YA WATOA HUDUMA ZA FEDHA KITAIFA
T-PESA, Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), imehitimisha ushiriki wake katika Maadhimisho ya Wiki ya Watoa Huduma za Fedha Kitaifa kwa mafanikio makubwa baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika kundi la kampuni zinazotoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, yakianza rasmi tarehe 19 Januari na kuhitimishwa Januari 26, 2026 yakiwa na kauli mbiu inayohimiza ujumuishi wa huduma za kifedha na matumizi ya huduma za fedha za kidijitali kwa maendeleo ya wananchi.
Katika kipindi chote cha maadhimisho hayo ya kitaifa, T-PESA ilishiriki kikamilifu kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zake, kujibu maswali ya wateja pamoja na kuhamasisha matumizi salama na rahisi ya huduma za fedha kupitia mitandao ya simu.
Ushiriki huo umeiwezesha T-PESA kuonesha mchango wake katika kukuza ujumuishi wa kifedha, hususan kwa kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutumia huduma za kifedha za kidijitali katika shughuli zao za kila siku.
Katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo, T-PESA ilikabidhiwa tuzo ya mshindi wa tatu na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Burian, ambaye aliipongeza kampuni hiyo kwa ushiriki wake wa dhati na mchango wake katika kufanikisha maadhimisho hayo ya kitaifa.
Tuzo hiyo ni ishara ya kutambua juhudi za T-PESA katika kuboresha huduma zake na kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa sekta ya fedha katika kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.
Kupitia ushindi huo, T-PESA imeahidi kuendelea na dhamira chanya ya kutoa huduma bora, salama na nafuu za kifedha kwa wananchi, sambamba na kuchangia jitihada za kitaifa za kukuza matumizi ya teknolojia katika huduma za fedha kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.