T-PESA YADHAMINI NA KUSHIRIKI SEMINA YA UONGOZI WA WANAWAKE KATIKA BIMA BARANI AFRIKA
Kampuni ya T-Pesa imedhamini na kushiriki kikamilifu katika Semina ya Uongozi wa Wanawake katika Bima Barani Afrika (Women Leadership in Insurance Africa), iliyofanyika Novemba 14 mwaka huu katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam.
Semina hiyo ilibeba kaulimbiu yenye nguvu na yenye kutia hamasa: “Empowered to Lead: Women Shaping the Future.” Kaulimbiu hii ilijikita katika kuonesha mchango mkubwa wa wanawake katika Sekta ya Bima, Fedha na Teknolojia pamoja na kuhamasisha uwezeshaji endelevu wa wanawake katika nafasi za maamuzi na uongozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa T-Pesa, Bi. Happy Nzunda, alimpongeza Mkurugenzi wa Women Leadership in Insurance Africa Bi. Lorna Mbwette kwa kuandaa jukwaa muhimu linaloendelea kumpa mwanga na dira mwanamke wa Kiafrika katika safari yake ya kujikwamua kiuchumi,
Bi Nzunda alisema kuwa T-Pesa inaamini katika nguvu, weledi na ubunifu wa wanawake, hivyo imekuwa ikihakikisha wanapewa kipaumbele katika nafasi mbalimbali za kiutendaji.
Aidha, aliongeza kuwa ushiriki wa T-Pesa katika semina hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni hiyo katika kuimarisha usawa wa kijinsia, kuendeleza vipaji vya wanawake, na kuchochea ubunifu kupitia mitazamo mipya inayochangiwa na uongozi wa wanawake.
Semina hiyo iliwakutanisha viongozi wa sekta ya bima na fedha kutoka Taasisi na Mashirika binafsi nchini , ambapo walijadili namna ya kuvunja vizuizi na changamoto zinazowakabili wanawake katika maeneo yao ya kazi na changamoto za mwanamke wa kisasa katika kutafuta usawa.
Ushiriki wa T-Pesa katika mkutano huo unaonesha kwamba kampuni hiyo ni mdau muhimu katika kujenga jamii jumuishi inayoweka mbele maendeleo ya wanawake.