info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

RIDHIWAN KIKWETE ATEMBELEA BANDA LA TTCL, AFUNGA RASMI MKUTANO WA 6 WA SERIKALI MTANDAO AICC

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, ametembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Mkutano wa 6 wa Serikali Mtandao uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha International Conference Centre (AICC), jijini Arusha.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Ridhiwani alipata fursa ya kujionea huduma na mifumo mbalimbali ya kidijitali inayotolewa na TTCL kwa taasisi za umma na binafsi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete alifunga rasmi mkutano huo wa siku tatu uliowakutanisha wadau wa TEHAMA wapatao 400 kutoka serikalini na sekta binafsi, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, aliwataka Wakuu wa Taasisi na Idara za Serikali kuendelea kutoa nafasi kwa wafanyakazi wao kujifunza na kujiendeleza katika eneo la TEHAMA. Alieleza kuwa kuendelea kupata ujuzi zaidi katika TEHAMA kutawawezesha watumishi wa umma kuwa wabunifu, kuongeza ufanisi kazini, na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

“Mabadiliko ya teknolojia ni ya haraka sana; hivyo ni wajibu wa viongozi kuhakikisha watumishi wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuendana na kasi hiyo na kuleta matokeo chanya katika utendaji wa serikali,” alisisitiza.

Mkutano huo wa 6 wa Serikali Mtandao umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuonesha ubunifu wa kidijitali, na kujadili mikakati ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA serikalini kwa lengo la kujenga serikali yenye ufanisi, uwazi na inayowajibika zaidi kwa wananchi.

Mkutano wa mwaka huu uliongozwa na kauli mbiu isemayo; "Kuboresha Utendaji wa Serikali kwa Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Umma Kupitia Mifumo Salama na Jumuishi ya Serikali Mtandao”