
NAIBU WAZIRI MKUU ATEMBELEA BANDA LA TTCL AICC ARUSHA
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ametembelea Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wakati wa hafla ya kufunga Kikao Kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC jijini Arusha.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mkuu alipokelewa na wataalamu wa TTCL akiwemo Afisa Mauzo Mwandamizi, Bw. Jumanne Mangube, ambaye alitoa maelezo ya kina kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo. Huduma hizo ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (National Data Centre) ambazo zimekuwa nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Bw. Mangube alieleza kuwa kupitia Mkongo wa Taifa, TTCL imeweza kuunganisha Taasisi za Umma, Mashirika Binafsi na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano ndani na nje ya nchi, hali inayochangia kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano.
Aliongeza kuwa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data ndiyo msingi imara wa usalama wa taarifa, uhifadhi salama wa mifumo ya kiserikali na kibiashara, pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kidijitali.
Aidha, Afisa huyo alisisitiza dhamira ya TTCL ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati na kuhakikisha huduma zake zinawafikia Watanzania wengi Zaidi ambapo sasa shirika hilo limejipanga kuimarisha huduma za TEHAMA ili kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa ajenda ya serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na kukuza ushindani wa Taifa kupitia uchumi wa kidigitali.
Ziara hii imekuwa fursa kwa Naibu Waziri Mkuu kuona namna shirika hilo linavyotekeleza majukumu yake ya kitaifa kwa vitendo na namna linavyoshirikiana na Mashirika ya Umma katika huduma zake kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Data, ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
Kikao kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma kimefungwa rasmi Agosti 26 mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC Arusha, kililenga kujadili namna ya kuongeza uwajibikaji, uwazi, tija na mchango wa mashirika ya umma katika maendeleo ya Taifa.