info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

NAIBU WAZIRI MKUU AKABIDHI CHETI CHA UTAMBUZI KWA TTCL

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amemkabidhi cheti cha shukrani Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa shirika hilo katika kudhamini Kikao Kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma. Hafla hiyo imefanyika leo, Agosti 26 mwaka huu wakati wa kufungwa rasmi kwa kikao hicho katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC jijini Arusha.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vyeti kwa wadhamini na washiriki mbalimbali, Mhe. Dkt. Biteko alitoa hotuba yenye kuhamasisha viongozi wa mashirika ya umma kuongeza kasi katika uwajibikaji, utendaji na ufanisi. 

Alisisitiza kuwa serikali inatarajia taasisi zote za umma ziwe mfano bora wa usimamizi wa rasilimali za nchi, kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za serikali, uwazi na weledi, ili kuendana na kasi ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri Mkuu aliwapongeza Viongozi na wadau wote walioshiriki kikao hicho na kuwataka kutambua kuwa serikali inawategemea hivyo majadiliano na madhimio waliyoyaweka yatasaidia kuleta chachu katika kuendeleza Taifa. 

“…Kwa kutumia fursa hii ya kuwa nanyi leo kwenye tukio hili muhimu kuwa Mhe. Raisi anatarajia makubwa kutoka kwenu kwakuwa mmeishaanza kuyaonesha na anatarajia mengi Zaidi na wananchi pia wanatarajia mengi kutoka kwenu” Alisema Dkt. Biteko

TTCL inaendelea kushirikiana na serikali na taasisi zote za umma katika kuimarisha huduma za mawasiliano na TEHAMA ili kuhakikisha huduma za kidijitali zinawafikia Watanzania wengi zaidi, sambamba na kuchangia ufanisi wa mashirika ya umma.

Udhami wa TTCL katika kikao hiki ni mwendelezo wa kuthibitisha dhamira ya shirika hilo kushirikiana na serikali katika kufanikisha vikao vya kimkakati vinavyolenga kuimarisha uongozi, uwajibikaji na tija katika sekta ya umma. 

Kikao kazi cha Tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi kiliwakutanisha viongozi waandamizi wa serikali na taasisi mbalimbali za umma kwa siku siku nne kuanzia Agosti 23 hadi 26 mwaka huu lengo kuu lilikuwa ni kujadili mikakati ya kuongeza uwajibikaji, tija na mchango wa mashirika ya umma katika maendeleo ya Taifa, huku pia kikitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuimarisha mshikamano wa viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

.