NAIBU WAZIRI MKAMA AHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA VIONGOZI NA WATUMISHI SEKTA YA MAWASILIANO
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Switbert Mkama amehimiza Uwajibikaji kwa Viongozi,Bodi na Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.
Ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa hotuba ya kufunga Mafunzo maalum ya Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Taasisi zake yaliyofanyika katika Viwanja vya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari jijini Dodoma.
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo wa kiuongozi, maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo, Dkt. Mkama alisisitiza kuwa uongozi wa kimkakati ni zaidi ya kusimamia shughuli za kila siku ni uwezo wa kuwa na maono, kupanga kwa weledi na kusimamia mabadiliko hususan katika kipindi hiki cha mageuzi ya kidijitali.
Aidha, mafunzo hayo yamegusa masuala muhimu ya itifaki za Serikali, maadili ya utumishi wa umma, pamoja na umuhimu wa kuzingatia taratibu rasmi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ili kulinda hadhi ya taasisi za umma.
Kwa upande wa ustawi wa watumishi, washiriki walipata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuwa afya njema kwani ndiyo msingi wa utendaji bora na maendeleo ya taasisi.
Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuamini kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea viongozi wenye maadili, ujuzi na afya njema.