info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MWENYEKITI WA BODI YA UCSAF AVUTIWA NA UBUNIFU WA TTCL SABASABA 2026

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Balozi Valentino Longino Mlowola, ametembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Balozi Mlowola alipata fursa ya kujionea huduma na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC), pamoja na huduma ya WiFi katika Maeneo ya Umma (Public WiFi), ambayo inaendelea kupanua upatikanaji wa intaneti katika maeneo muhimu nchini, yakiwemo Mlima Kilimanjaro, taasisi za elimu na stendi za mabasi.

Aidha, alitembelea FTTX Experience Center, ambapo alipata maelezo kuhusu huduma ya Faiba Mlangoni Kwako, inayowezesha wananchi na wafanyabiashara kupata intaneti ya kasi, salama na yenye uhakika kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Balozi Mlowola aliipongeza TTCL kwa maandalizi na ubunifu uliotumika katika kuwasilisha huduma zake kwenye maonesho hayo. Alisema banda la TTCL limekuwa jukwaa muhimu linalowapa wananchi na wadau fursa ya kujifunza kuhusu mchango wa teknolojia ya mawasiliano katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa kidijitali nchini.

TTCL inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba 2026 kama fursa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma zake za kisasa na suluhisho za TEHAMA, huku ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote na kuchangia safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.