info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MWENGE WA UHURU WAIPONGEZA TTCL: KITUO CHA MKONGO KUWA MWOKOZI WA MAWASILIANO SIKONGE NA MAENEO YA JIRANI

Katika muendelezo wa kutekekeleza agenda ya Serikali ya Tanzania ya Kidigitali, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepokea pongezi za Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kwa juhudi zake thabiti za kusambaza huduma bora za mawasiliano kwa Wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, alipokuwa akiweka Jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wilayani Sikonge, mkoani Tabora.

Akizungumza mbele ya Viongozi wa Chama na Serikali, wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo Ussi amesema Mradi huo wa kituo cha mkongo utaleta mapinduzi makubwa sio tu Sikonge bali pia maeneo ya jirani

hatua ambayo inatazamwa kama kichocheo kikuu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.

“Tunawapongeza TTCL kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuunganisha Watanzania kupitia huduma bora za mawasiliano kwani kituo hiki kitakuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo haya,” amesema Ndg. Ussi 

Kituo hiki cha mkongo kimejengwa kwa lengo la kuongeza uwezo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kasi na ya uhakika kwa wananchi wa Sikonge na Mikoa ya jirani. 

Mradi huu ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuijenga Tanzania ya kidijitali kupitia miundombinu ya mawasiliano inayowafikia wananchi vijijini na mijini.

Kupitia kituo hiki Wananchi watanufaika na huduma za intaneti zenye kasi na gharama nafuu, jambo litakalorahisisha upatikanaji wa taarifa, elimu, huduma za afya kwa njia ya mtandao, pamoja na fursa za kiuchumi kupitia biashara mtandao.

Aidha Taasisi za Umma na Binafsi kama Shule, Hospitali, Vituo vya Polisi, na Mahakama zitawezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa haraka na hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mwenge wa Uhuru ukiwa kama alama ya mshikamano wa kitaifa na maendeleo ya kijamii, umekuwa ukisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo endelevu. 

Uwekaji wa jiwe la msingi katika kituo cha mkongo Sikonge si tu ishara ya kuunga mkono juhudi za TTCL, bali pia ni mwito kwa jamii kutumia kikamilifu miundombinu hiyo kwa maendeleo yao.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa TTCL Mkoa wa Tabora, Bw. Charles Msoma ameeleza kuwa ujenzi wa kituo hiki ni sehemu ya mkakati mpana wa TTCL kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kila mahali nchi nzima ili kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma bora zinazokwenda sambamba na kasi ya Dunia ya kidijitali.