
MPANGO MKAKATI WA SHIRIKA: UNALENGA KUJIENDESHA KWA TIJA NA UFANISI
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limewasilisha rasmi Mpango Mkakati wa Biashara wa Miaka Mitatu (2025/26 – 2027/28) mbele ya Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, katika kikao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Mohammed Khamis Abdulla.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali – Mtumba, Dodoma.
Akiwasilisha mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alieleza kuwa mpango huu mpya umeandaliwa kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi kupitia huduma bora, za kisasa na zenye uhakika za mawasiliano ya kidijitali, sambamba na kuimarisha ushirikishwaji wa kidijitali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
“Kupitia mkakati huu, TTCL inalenga kuwa Shirika linalojiendesha kwa tija na ufanisi, lenye muonekano mpya wa kisasa, na hatimaye kuanza kutoa gawio kwa Serikali kama sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya Taifa,” alisema Marwa.
Mpango huo unaweka msingi wa mabadiliko makubwa ndani ya Shirika, ukiakisi dhamira ya TTCL kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) duniani, huku ukilenga kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma bora, jumuishi na zenye gharama nafuu.