info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MKURUGENZI MTENDAJI T- PESA AONGOZA JUKWAA LA WANAWAKE SABASABA 2024

Wanawake Viongozi kutoka kwenye Taasisi, Kampuni, Mashirika, Wajasiriamali na Wafanyabiashara wamekutana katika jukwaa la Wanawake katika Uongozi (Women in Leadership Forum) kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Jukwaa hili lilifanyika Julai 12, 2024 katika Ukumbi wa Dome uliopo Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo lililenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania. 

Jukwa hili lilifanyika wakati Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara kwa mwaka huu 2024 yakiendelea ambapo maonesho haya yamekuwa fursa nzuri kwa wanawake kupata mafunzo, kujenga mtandao, na kushiriki katika mijadala inayolenga kuimarisha nafasi yao katika jamii na uchumi.

Katika jukwaa hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya T- Pesa ya Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL, Bi Lulu Mkudde alikuwa miongoni mwa Wanawake Viongozi walioshiriki katika jukwaa hilo ambapo alisema kuwa pamoja na mambo mengine jukwaa hilo ni fursa ya kushirikishana uzoefu katika nyanja mbalimbali na namna ya kukabiliana na changamoto katika uongozi wao. 

“Jukwaa hili lengo lake ilikuwa ni kutoa fursa kwa wanawake kujifunza, kushirikiana, na kusaidiana katika kukuza uwezo kwenye nyanja za uongozi, biashara, na maendeleo ya jamii” alisema Lulu 

Alisema jukwaa la Wanawake katika uongozi ni muhimu sana kwa sababu linatoa fursa na mazingira salama kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na hivyo kuongeza Usawa na Uwakilishi katika nafasi za uongozi.

Aliongeza kuwa Wanawake wanapokutana katika majukwaa kama haya uweza kuwa chanzo cha hamasa, kuleta ubunifu, kuleta suluhisho jipya kwa changamoto za kiuongozi kwa wanawake wengine kuchukua hatua za kiuongozi na kujiamini zaidi katika majukumu yao ya uongozi na kuleta mabadiliko endelevu katika sera za kampuni au serikali. 

“Kwakutumia majukwaa kama haya Wanawake wanaweza kuleta ubunifu na suluhisho mpya kwa changamoto za kiuongozi na kijamii na kuwa sehemu ya ujenzi wa jamii yenye usawa ujuzi na mafanikio makubwa zaidi kwa kuzingatia na kuheshimu uwezo wa wanawake katika nafasi za uongozi” alisema.