MKURUGENZI MKUU WA TTCL AKAGUA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO NA MIRADI YA UPANUZI WA FAIBA PEMBA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, amefanya ziara ya kukagua miundombinu mbalimbali ya mawasiliano katika Mkoa wa Pemba ikiwa ni sehemu ya jitihada za Shirika za kuhakikisha uwekezaji uliofanywa katika sekta ya mawasiliano unaleta tija, unaimarisha huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Katika ziara hiyo, Bw. Marwa alitembelea vituo vya minara ya mawasiliano vilivyojengwa kupitia mradi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ikiwemo Kituo cha Mgelema, ambapo alipata fursa ya kujionea hali ya utoaji wa huduma na maendeleo ya matumizi ya miundombinu hiyo katika kuhudumia wananchi wa maeneo husika.
Mkurugenzi Mkuu huyo pia alikagua kituo kikuu cha huduma za Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) kilichopo Michakaini, Wete, ambacho kina umuhimu mkubwa katika kuunganisha na kusambaza huduma za mawasiliano kati ya maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa Pemba.
Akizungumza na watendaji wa vituo hivyo, Bw. Marwa alisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu miundombinu iliyopo kwa kuongeza matumizi ya huduma za mawasiliano, kuvutia wateja wapya na kuimarisha mapato yatokanayo na uwekezaji uliofanywa na Shirika.
“TTCL imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya mawasiliano. Ni wajibu wetu kuhakikisha uwekezaji huu unaleta manufaa kwa wananchi na Shirika kwa kuongeza matumizi ya huduma zetu na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kidijitali katika maeneo yote tunayohudumia,” alisema Bw. Marwa.
Aliongeza kuwa kutokana na ukubwa wa gharama za uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya mawasiliano ni vyema kuongeza juhudi za kibiashara na kuhamasisha matumizi ya huduma zinazotolewa kupitia miundombinu hiyo ili kuhakikisha uwekezaji unaendelea kuwa endelevu na wenye tija.
Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Bw. Marwa alitembelea eneo la Kifumbikai, Wete, ambapo alikagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Gigabit Passive Optical Network (GPON) unaolenga kupanua huduma za intaneti ya kasi kwa wananchi.
Kupitia mradi huo, jumla ya Home Pass 1,024 zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Wete, huku Home Pass 2,048 zikitarajiwa kujengwa katika eneo la Chake Chake. Utekelezaji wa mradi huo utaongeza upatikanaji wa huduma za Faiba Mlangoni Kwako na kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za intaneti ya kasi na uhakika.