info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MKURUGENZI MKUU TTCL ATEMBELEA MABANDA YA TAASISI ZA MBALIMBALI SABASABA 2026

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),  Moremi Marwa, ametembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), kwa lengo la kujionea ubunifu wa teknolojia, kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kutambua fursa zinazoweza kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.

Katika ziara hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Marwa alitembelea mabanda ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ambapo alipata maelezo kuhusu tafiti, ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazoendelea kuendelezwa na taasisi hizo.

Akiwa katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mkurugenzi Mkuu alipata fursa ya kujionea teknolojia rafiki kwa mazingira ya ujenzi iliyobuniwa na Idara ya Kemia chini ya uongozi wa Dkt. Makungu Marco Madirisha. Ubunifu huo unalenga kuzalisha matofali na paving blocks nyepesi lakini imara kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini, hatua inayotoa suluhisho endelevu na lenye gharama nafuu kwa sekta ya makazi na maendeleo ya miundombinu.

Akizungumza baada ya kutembelea bunifu hiyo, Bw. Marwa alisema uvumbuzi huo unaonesha uwezo mkubwa wa taasisi za elimu ya juu nchini katika kuzalisha suluhisho za vitendo zinazotokana na tafiti za ndani.

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti, sekta ya viwanda na taasisi za umma ili bunifu hizo ziweze kufikishwa sokoni, kuongeza thamani ya tafiti zinazofanyika nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi pamoja na maendeleo ya kijamii.

Katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Bw. Marwa alipata maelezo kuhusu maendeleo ya mradi wa kubuni na kurusha setilaiti unaotekelezwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Alipongeza hatua zilizofikiwa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia za anga, akieleza kuwa teknolojia hizo zina nafasi kubwa katika kuimarisha mawasiliano, usimamizi wa taarifa na maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.

Aidha, alipotembelea banda la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), alipata fursa ya kujadili maendeleo ya sekta ya mawasiliano na nafasi ya teknolojia katika kuimarisha utoaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za TTCL za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na wadau mbalimbali, kubadilishana uzoefu, kutambua fursa za ubunifu na kuunga mkono utekelezaji wa ajenda ya Tanzania ya Kidijitali kupitia matumizi ya teknolojia na suluhisho bunifu kwa maendeleo endelevu ya Taifa.