info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MHE. KAIRUKI ATOA MAAGIZO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MIUNDOMBINU SHIRIKISHI KWA MAENDELEO YA TEHAMA

Waziri wa  Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angela Jasmini Mbelwa Kairuki (Mb), ametoa maagizo kwa taasisi zilizo chini ya Wizara anayoiongoza na Wadau wa Sekta Binafsi kuimarisha ushirikiano wa kimkakati utakaochochea uwekezaji, ubunifu na upanuzi wa huduma za mawasiliano nchini ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, salama na zenye tija katika zama za uchumi wa kidijitali.

Maagizo hayo yametolewa hivi karibuni jijini Dodoma wakati wa Kikao Kazi kilichowakutanisha Wizara, Taasisi na Bodi zilizo chini yake pamoja na Wadau wa Sekta Binafsi kwa lengo la kujadili maendeleo ya TEHAMA na mawasiliano nchini. 

Waziri Kairuki alisisitiza kuwa mashauriano ya mara kwa mara ni nyenzo muhimu ya kutatua changamoto na kuweka dira ya pamoja ya maendeleo ya sekta.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria ili kuvutia uwekezaji zaidi katika miundombinu ya mawasiliano huku akizitaka Taasisi na Kampuni binafsi kushirikiana katika miradi ya kimkakati itakayopanua upatikanaji wa huduma za intaneti na mawasiliano vijijini na mijini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. David Nchimbi, aliishukuru Wizara kwa kuandaa kikao hicho akibainisha kuwa ni jukwaa muhimu la kujenga uelewano na kuweka mikakati ya pamoja. Amesema TTCL itaendelea kushirikiana na taasisi za umma na sekta binafsi kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.

Aidha, Bw. Nchimbi aliiomba Wizara kuendelea kuboresha sera zitakazowezesha utekelezaji wa dhana ya miundombinu shirikishi (shared infrastructure). Amefafanua kuwa katika utekelezaji wa miradi ya miji janja (Smart City), ni muhimu kuwepo kwa mifumo ya pamoja ya njia za chini ya ardhi (ducts) zitakazoweza kupitisha kwa pamoja huduma za maji, umeme, mawasiliano na gesi ili kupunguza gharama na uharibifu wa mara kwa mara wa miundombinu.

Kikao kazi hicho kilikuwa ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Wizara za kuimarisha mashauriano na wadau, kuchambua mafanikio na changamoto za sekta, pamoja na kuweka mikakati madhubuti itakayohakikisha mawasiliano na TEHAMA vinaendelea kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini