info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MHE. KAIRUKI ATEMBELEA KITUO CHA MAONESHO KIJITONYAMA, KUSHUHUDIA UBUNIFU WA TEKNOLOJIA YA FTTX

Na Adeline Berchimance

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na huduma za mawasiliano zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), hususan huduma za intaneti ya kasi kupitia Faiba Mlangoni Kwako, ili kuongeza matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku na kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo, Septemba 15, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha maonesho cha Huduma za Faiba (FTTX) kilichopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, ambako alikagua na kupata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL kituoni hapo.

Waziri Kairuki amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya TEHAMA, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa ajili ya maendeleo yao binafsi, kijamii na kiuchumi.

Amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza na kupata huduma za TTCL, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali una maana zaidi pale unapoweza kutumiwa na wananchi katika kuboresha maisha na kuongeza shughuli za kiuchumi.

Katika hatua nyingine amepongeza TTCL kwa kuendelea kupanua miundombinu ya mawasiliano na kuanzisha huduma zinazokwenda sambamba na mahitaji ya teknolojia ya sasa, ikiwemo Faiba Mlangoni Kwako na Smart Home, zinazolenga kuwawezesha wananchi kupata intaneti ya kasi majumbani, maofisini na katika maeneo ya biashara.

 “Niwapongeze sana TTCL kwa hatua kubwa mnazoendelea kuchukua katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za mawasiliano zenye kasi, uhakika na ubora,” amesema Mhe. Kairuki. 

Aidha, ameitaja TTCL kuwa miongoni mwa taasisi muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kukuza uchumi wa kidijitali, kutokana na nafasi yake katika kujenga na kuendesha miundombinu ya mawasiliano inayowawezesha wananchi kupata huduma za kidijitali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, amesema Shirika limeendelea kuongeza uwezo wa miundombinu yake ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwamba kwa sasa TTCL tayari imejenga uwezo wa takribani maunganisho takribani 330,000, takribani 400,000, hatua ambayo itafanya idadi ya maungio kufikia karibu 750,000 katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema utekelezaji wa mpango huo utaongeza uwezo wa TTCL kufikisha huduma za Fiber kwa wananchi wengi zaidi, huku hadi sasa takribani maunganisho 115,000 yakiwa tayari yameunganishwa na kutumia huduma hii na mpango uliopo ni kuhakikisha shirika linabaki kinara katika utoaji wa huduma ya intaneti kwa wananchi 

Amesema TTCL itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Fiber ili kuhakikisha uwekezaji uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya mawasiliano unawafikia wananchi moja kwa moja huku akisema kwa sasa TTCL inatumia teknolojia ya GPON katika utoaji wa huduma za FTTH, ambayo imechukua nafasi ya teknolojia ya awali ya Point-to-Point ambayo inawezesha kuunganisha wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Marwa amesema TTCL inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwawezesha Watanzania kushiriki katika uchumi wa kidijitali kupitia upatikanaji wa muunganisho wa intaneti na huduma mbalimbali zinazotegemea teknolojia.