
MAWAZIRI WAVUTIWA NA BANDA LA TTCL MKUTANO MKUU WA 14 WA AfIGF
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb) ameongoza msafara wa Mawaziri kutoka Mataifa mbalimbali ya Afrika kutembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (Africa Internet Governance Forum – AfIGF 2025), uliofanyika Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Mei 30 mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Mhe. Silaa pamoja na Mawaziri wenzake walipata fursa ya kujionea teknolojia za kisasa zinazotumiwa na TTCL katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini, hususan katika kuimarisha miundombinu ya mtandao wa intaneti na mawasiliano ya data.
Wakiwa katika banda hilo walionesha kuridhishwa na jitihada za serikali kupitia TTCL katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na za kisasa za mawasiliano na kutoa huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa nchi jirani kama Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi Malawi, Zambia na DRC ILI KUCHOCHEA matumizi ya TEHAMA katika nchi hizo na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Maafisa Mauzo wa shirika hilo waliwaeleza Mawaziri hao kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo ikiwa ni pamoja na huduma za fiber, huduma za mobile, huduma za data kwa taasisi, mashirika, kampuni mbalimbali za serikali na sekta binafsi, huduma ya Data Center na usambazaji na uuzaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
Mkutano huo wa AfIGF uliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano na teknolojia kutoka Afrika na kujadili masuala muhimu yanayohusu utawala wa mtandao, sera za kidijitali, usalama wa mtandao, na ujumuishwaji wa kijinsia na makundi maalum katika zama za teknolojia ya habari.
Ushiriki wa TTCL katika mkutano huu mkubwa wa bara la Afrika imekuwa fursa muhimu ya kukutana na wadau na kuonesha uwezo na mafanikio katika sekta ya mawasiliano na kuonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuwa chachu ya mageuzi ya kidijitali nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.