
KONGAMANO LA BIASHARA OSAKA, JAPAN: TTCL YAWAITA WAWEKEZAJI KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetumia fursa ya Kongamano la Biashara linalofanyika jijini Osaka, Japan kuanzia tarehe 25 hadi 26 Mei 2025, kuwavutia wawekezaji wa kimataifa kuwekeza katika sekta ya mawasiliano nchini Tanzania.
Mgeni Rasmi wa Kongamano hilo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), na kuhudhuliwa na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania na Japan, wawekezaji, na wadau muhimu kutoka sekta binafsi.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, alitumia jukwaa hilo kuwasilisha miradi ya kimkakati na kuwaalika wawekezaji wa Kimataifa kushirikiana na TTCL katika kuendeleza sekta ya mawasiliano nchini.
“Lengo kuu la ushiriki wetu ni kutafuta fursa za kuimarisha ushirikiano katika kukuza teknolojia, kuboresha miundombinu ya mawasiliano, na kuendeleza huduma jumuishi za kidijitali nchini Tanzania,” alisema Bw. Marwa.
Akisisitiza nafasi ya Tanzania kama kitovu cha mawasiliano barani Afrika, Bw. Marwa alieleza kuwa Tanzania ni lango muhimu la mawasiliano katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni mahali sahihi kwa uwekezaji wa kiteknolojia wenye tija.
Ushiriki wa TTCL katika Kongamano la Biashara la Osaka ni uthibitisho wa dhamira ya Tanzania katika kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuendeleza sekta ya mawasiliano ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidijitali duniani.