KIZIMKAZI 2026 YAFIKIA KILELE LEO ZANZIBAR, MHE. RAIS AFUNGA RASMI
Na Godfrey Andafiche
Tamasha la Kizimkazi 2026 limefikia kilele chake leo katika Viwanja vya Makunduchi, Zanzibar, likihudhuriwa na kufungwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tamasha hilo limewakutanisha wananchi, viongozi, taasisi, kampuni, mashirika ya umma na wafanyabiashara mbalimbali, likiendelea kujidhihirisha kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha jamii na fursa za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Sambamba na Tamasha hilo, yamefanyika maonesho ya kibiashara yaliyoshirikisha zaidi ya taasisi, kampuni na mashirika ya umma 120, pamoja na zaidi ya wajasiriamali 200, waliopata nafasi ya kuonesha bidhaa, huduma na ubunifu wao kwa wananchi na wageni waliohudhuria.
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekuwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika Kizimkazi 2026 kupitia banda lake, ambapo wananchi na wageni walipata fursa ya kujifunza, kupata taarifa na kufahamu huduma na suluhisho mbalimbali za mawasiliano zinazotolewa na Shirika.
Kupitia ushiriki huo, TTCL imeonesha namna teknolojia na huduma za mawasiliano zinavyoweza kurahisisha maisha ya wananchi, kuimarisha shughuli za biashara na kufungua fursa mpya katika uchumi unaoendelea kuelekea katika matumizi makubwa ya teknolojia za kidijitali.
Uwepo wa TTCL katika Tamasha la Kizimkazi 2026 pia umeendelea kuimarisha dhamira ya Shirika ya kuwa karibu na wateja, kusikiliza mahitaji yao na kushiriki kikamilifu katika matukio ya kitaifa yanayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tamasha la Kizimkazi limeendelea kuwa moja ya majukwaa yanayotoa nafasi kwa taasisi, sekta binafsi na wajasiriamali kukutana moja kwa moja na wananchi, kujenga mitandao ya biashara, kutangaza huduma na bidhaa pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu fursa mbalimbali za maendeleo.
Kwa TTCL, ushiriki katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kusogeza huduma za mawasiliano karibu zaidi na Watanzania na kutumia teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuunganisha watu, biashara na fursa za maendeleo nchini.