info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

KICHERE AWAPONGEZA WANAWAKE, ASEMA SHIRIKA LINAWATAMBUA

Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wameungana na maelfu ya wanawake kutoka sekta mbalimbali kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Kitaifa jijini Arusha.

Maadhimisho hayo, yenye kaulimbiu "Wanawake na Wasichana 2025, Tuimarishe Haki, Usawa na Uwajibikaji" yamefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha huku Mgeni rasmi akiwa Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

TTCL ilitumia maadhimisho haya kuonesha na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia na mawasiliano kupitia Banda la maonesho lilikuwepo katika maeneo uwanja huo.

Katika banda hilo Wanawake hao walitoa elimu ya uelewa na  kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya mawasiliano katika kuboresha maisha ya jamii. 

Aidha walitoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za kidijitali zinazotolewa na TTCL, zikiwemo huduma za intaneti ya kasi, mawasiliano ya simu, na suluhisho la TEHAMA kwa biashara na ujasiriamali.

Katika hatua nyingine Meneja Mkoa wa Arusha Bw. Iman Kichere alifanya mazungumzo na Wanawake hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwahudumia wananchi.

Alisema Shirika linatambua kazi inayofanywa na Wanawake wote ya uhandisi, Sheria, uhasibu, ukatibu Mhutasi na kazi zote zinazotekelezwa na wanawake kupitia idara mbalimbali.

Aliwataka kutojibweteka bali waendelee kuonesha uwezo walionao kwa kufanya kazi kibunifu huku wakizingatia weledi wa taaluma zao.

Naye Mercy Aman Mwenyekiti wa Wanawake TTCL aliishukuru Menejimenti kwa kulisimamia Shirika kimkakati na kuhakikisha linafanya kazi ya ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ili huduma ya mawasiliano na TEHAMA izidi kuimarika nchini.

Alisema Menejimenti imekuwa bega kwa bega na Wanawake wa Shirika hilo kila mwaka kuhakikisha wanashiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani kilimalizika Machi 8, 2025 kwa Wanawake kutoka Taasisi, Mashirika ya umma na binafsi pamoja na Kampuni za kiserikali na binafsi kuandamana wakiwa na ujumbe mbalimbali unaoakisi kufurahia na kuendelea kuchochea amasa za kumkomboa mwanamke kifkra ili kumletea maendeleo endelevu.

.