
HUDUMA BORA KWA WATEJA NDIYO DIRA YA TTCL – Bi. ANITA MOSHI
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, ikiambatana na kaulimbiu ya mwaka huu: “Mission: Possible.”
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi uliofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TTCL, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Bi. Anita Moshi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kujitathmini, kusikiliza wateja kwa makini, na kuboresha huduma kwa ufanisi zaidi.
“Wiki hii ni alama muhimu katika kalenda yetu. Inatukumbusha wajibu wetu wa msingi kumweka mteja mbele kama kiini cha mafanikio ya TTCL,” alisema Bi. Moshi.
Alisema kaulimbiu ya “Mission: Possible” inatoa nguvu mpya kwa Watumishi wa TTCL kuona kila changamoto kama fursa ya kuboresha huduma, kubuni suluhisho bunifu, na kuimarisha uhusiano wa kudumu na wateja.
Bi. Moshi aliongeza kuwa kupitia Mpango Mkakati wa TTCL, shirika limejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini, ikiwa ni pamoja na kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikia wilaya zote, pamoja na ujenzi wa minara 1,400 katika maeneo ya vijijini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za mawasiliano bila vikwazo.
Alibainisha kuwa TTCL inaendelea pia kusambaza huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako,” inayowezesha wateja kupata intaneti ya kasi na ya uhakika majumbani, mashuleni, na katika taasisi mbalimbali nchini.
“Tunataka kila Mtanzania anufaike na huduma bora za mawasiliano. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kuboresha mifumo ya huduma, na kuhakikisha kila mteja anasikilizwa, anathaminiwa, na anahudumiwa kwa ubora wa hali ya juu,” alisisitiza Bi. Moshi.
Aidha, aliwahimiza wateja wa TTCL kuendelea kutumia Kituo cha Huduma kwa Wateja cha saa 24, mitandao ya kijamii, na Maduka ya TTCL yaliyopo nchi nzima ili kupata huduma, ushauri, au taarifa muhimu.
Aidha aliwashukuru wateja wote kwa kuendelea kuiamini TTCL, akisisitiza kuwa wao ndiyo msingi wa mafanikio ya shirika hilo.
“Tutaendelea kuwa bega kwa bega na wateja wetu katika safari hii ya maendeleo ya kidijitali. Kwa pamoja, tutafanikisha azma yetu ya mwaka huu — Mission: Possible,” Alisema Bi. Moshi
Wiki ya Huduma kwa Wateja ya TTCL itaendelea hadi Oktoba 10, 2025, ikiwa na shughuli mbalimbali za kutoa huduma, kusikiliza maoni ya wateja, na kuelimisha umma kuhusu huduma za shirika.