CPA MOREMI MARWA AKABIDHIWA OFISI RASMI
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL, CPA Moremi Marwa amekabidhiwa rasmi Ofisi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Hafla ya makabidhiano ilifanyika Agosti 15, 2024 baada ya mtangulizi wake, Mhandisi Peter Ulanga, kumaliza muda wake wa uongozi.
Katika hotuba yake ya kukabidhiwa ofisi, CPA Marwa alimshukuru mtangulizi wake kwa kazi aliyoifanya kwa kipindi chote alipokuwa Mkurugenzi Mkuu huku akiomba ushirikiano kutoka kwa Wafanyakazi wote wa TTCL ili kufanikisha malengo ya shirika hilo na kujenga msingi imara wa huduma bora kwa Watanzania.
Kwa upande wake Mhandisi Ulanga alimshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuliongoza Shirika hilo kwa kipindi cha Miaka Miwili na Miezi mitano.
Mhandisi Ulanga aliwashukuru Wafanyakazi, Serikali, na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake na alitumia jukwaa hilo kuisihi Menejimenti na Wafanyakazi wote kumpa ushirikiano wa kutosha Mkurugenzi Mkuu mpya ili kuliwezesha shirika kupiga hatua kwa haraka zaidi.
Aidha Mhandisi Ulanga aliwataka Wafanyakazi wa shirika hilo hasa Wahandisi kutotumia misamiati ya kitaalamu badala yake watumie lugha rahisi inayoweza kueleweka kwa urahisi ili utekelezaji wa majukumu ya uendeshaji wa shirika kuweza kutekelezeka.