info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI LAHIMIZWA KUIMARISHA MAHUSIANO YA KIKAZI ILI KULETA MWELEKEO CHANYA WA KIBIASHARA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limefanya kikao cha 12 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, mkoani Pwani, kikilenga kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya shirika, mahusiano ya kikazi na kujadili masuala ya ustawi wa Wafanyakazi na mwelekeo wa shirika kwa ujumla.

Kikao hicho kiliwakutanisha wajumbe wa Baraza Kuu, Menejimenti ya shirika hilo, Viongozi Vyama vya Wafanyakazi pamoja na Wawakilishi wa Wafanyakazi kutoka Mikoa mbalimbali ya kibiashara ya TTCL nchi nzima.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, alisema Baraza Kuu la Wafanyakazi ni chombo muhimu cha kuimarisha mahusiano ya kazi, kujenga mshikamano na kuongeza uelewano kati ya Viongozi na Wafanyakazi ndani ya shirika hilo.

Bw. Marwa aliwahimiza wajumbe wa baraza kuendelea kuimarisha mahusiano ya kikazi, kufanya kazi kwa mshikamano na kusisitiza kuwa bado kuna jukumu kubwa la pamoja la kulifikisha shirika katika malengo yake ya kimkakati. 

“TTCL inahitaji mawazo ya pamoja, uwajibikaji na ushirikiano wa dhati ili kusonga mbele katika mazingira ya ushindani” Alisema Marwa.

Alieza kuwa mpango mkakati wa miaka mitatu wa shirika hilo umejikita katika kuongeza ufanisi na tija kwa lengo la kuhakikisha TTCL inazalisha faida endelevu, na kuongeza kuwa shirika hilo lilianzishwa kwa dhamira ya kufanya biashara yenye faida na siyo kujiendesha kwa hasara.

Aidha alisisitiza umuhimu wa kila Mfanyakazi kuwajibika kikamilifu katika majukumu yake, kuimarisha mashirikiano kati ya viongozi na wafanyakazi wasiokuwa viongozi, pamoja na kuwa tayari kukabiliana na ushindani mkubwa wa kiteknolojia unaoendelea kukua katika sekta ya mawasiliano.

Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kujadili kwa kina masuala ya maendeleo ya shirika, kuboresha utendaji kazi na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi, huku kikilenga kuiandaa TTCL kukabiliana na changamoto na fursa za soko la mawasiliano linalobadilika kwa kasi.