
AfIGF FURSA MUHIMU KWA BARA LA AFRIKA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIJITALI – WAZIRI SILAA
Mkutano Mkuu wa 14 wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (Africa Internet Governance Forum - AfIGF) umefunguliwa rasmi leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa (Mb), alieleza kuwa mkutano huu ni fursa muhimu kwa bara la Afrika kuimarisha ushirikiano wa kidijitali, kuweka misingi madhubuti ya utawala bora wa mtandao na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika zama za mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali.
Jukwaa hili limewakutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Mawaziri na wawakilishi wa serikali kutoka zaidi ya nchi 30 barani Afrika, Mashirika ya kimataifa, Makampuni ya teknolojia kama, Wataalamu wa TEHAMA, wanaharakati wa haki za kidijitali, wanazuoni na wanafunzi.
Pamoja na mambo mengine Mkutano huo umelenga kujadili sera na sheria zinazohusiana na utawala wa mtandao barani Afrika, kukuza ushirikiano baina ya sekta binafsi, serikali, asasi za kiraia na taasisi za elimu katika masuala ya dijitali, kupendekeza mikakati ya kulinda haki za watumiaji wa mtandao, hasa katika maeneo ya faragha, usalama na uhuru wa kujieleza na kuweka msingi wa ushiriki wa vijana katika mapinduzi ya kidijitali barani Afrika.
Katika hatua nyingine Waziri Silaa aliongoza ujumbe wa Mawaziri na viongozi waandamizi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kutembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kabla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Jukwaa la Utawala wa Mtandao Afrika (AfIGF)
Ziara hiyo katika banda la TTCL ililenga kuona kwa karibu huduma na teknolojia zinazotolewa na shirika hilo nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuonesha mchango wa sekta ya mawasiliano katika kuimarisha utawala wa mtandao barani Afrika.
Mkutano wa AfIGF 2025 umehusisha mijadala ya kitaalamu na maonesho kutoka wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA, huku Tanzania ikitumia nafasi hiyo kuonesha mafanikio yake katika nyanja za mawasiliano na teknolojia kidigitali.