info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WATUMISHI TTCL WAPATIWA MAFUNZO YA SHERIA MPYA YA UNUNUZI WA UMMA

Watumishi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL wapatiwa mafunzo kuhusu Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake ikiwa ni katika kuhakikisha Watumishi wa Shirika hilo wanapata uelewa wa mabadiliko ya sheria ya mwaka 2023 na kanuni za ununuzi GN. No 518 za mwaka 2024.

Akiongea wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi za Makao makuu ya shirika hilo hivi karibuni, Mwezeshaji kutoka Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Furahael Lema alisema jukumu la Mamlaka hiyo kuhakikisha kila taasisi ya umma inatumia sheria mpya ya ununuzi ili kuleta tija katika utendaji na kufanya ununuzi kwa uadilifu na ufanisi.

Aidha aliongeza kuwa sheria na kanuni hizo zitasaidia kufanya maamuzi ya ununuzi bora na kupunguza hatari za kununua bidhaa zisizolingana na malengo ya Taasisi husika.

Naye Meneja Ununuzi na Ugavi wa TTCL Bw. Khamisi Madata ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa Idara ya Ununuzi kwani itasaidia katika kuhakikisha ununuzi unafanyika kwa kuzingatia uadilifu, ufanisi na kupata thamani halisi ya fedha katika kufanya ununuzi wa bidhaa mbalimbali zinazosaidia utendaji kazi wa Shirika.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yataongeza ufanisi na tija ndani ya Shirika kwa sababu sheria hiyo mpya imetoa vikwazo vingi vilivyokuwepo katika sheria ya zamani kurahisisha katika utekelezaji wake.

“Mafunzo haya yataongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa ununuzi ndani ya Shirika na kwa sasa tumeanza kuwapatia Watumishi wa Idara ya Ununuzi na Ugavi kisha tutaenda kwa Viongozi na Menejimenti (SMT) na Watumishi wengine wa Idara ndani ya Shirika.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa Shirika katika kuhakikisha watumishi wake wanapata mafunzo kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu kuimarisha utendaji wa Shirika.