
WASTAAFU TTCL WAISHUKURU MENEJIMENTI KWA KUWAPA MAFUNZO YA KUSTAAFU
Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL waliostaafu na wanaotarajia kustaafu hivi karibuni wameishukuru Menejimenti ya shirika hilo kwa kuwaandalia mafunzo maalum ya maandalizi ya kustaafu.
Akizungumza kwa niaba ya Wastaafu, mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Bwana Michael Nchimbi aliipongeza Menejimenti kwakuwaandalia mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo wa maisha baada ya kustaafu.
Alisema kuwa elimu waliyopewa itawasaidia kukabiliana na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uelewa kuhusu umuhimu wa kuwekeza mapema, kupanga bajeti kwa uangalifu, na kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii ili kudumisha afya ya mwili na akili.
Naye Bwana Bahida Magembe aliishauri Menejimenti kuyafanya mafunzo hayo kuwa endelevu na yapewe kipaumbele kwa wafanyakazi wengine wanaokaribia kustaafu, ili kuwaandaa vyema kwa maisha yajayo.
Mafunzo haya yamewapa ujuzi na mwongozo muhimu kuhusu jinsi ya kujiandaa kwa maisha baada ya utumishi, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa fedha, afya, na shughuli za maendeleo binafsi.
Menejimenti ya TTCL ilianzisha mpango huu ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuhakikisha Wafanyakazi wake wanastaafu kwa heshima na utulivu, huku wakipata maarifa ya kujimudu baada ya utumishi wao.