UKAGUZI WA MAENDELEO YA MRADI
Kamati Tendaji ya Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania limefanya ziara kukagua mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika vituo vya Msalala na Mbogwe,Ushirombo na Geita lengo likiwa ni kuangazia maendeleo ya mradi huo.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyeki wa Kamati hiyo Bw. Jalili Senkopwa ilipata fursa ya kujionea kazi iliyofanyika na kuipongeza Menejimenti ya TTCL kwa juhudi na kazi kubwa iliyofanyika mpaka sasa katika utekelezaji wa mradi huo.
Bw. Jalili alisema kuwa Shirika limefanya kazi kubwa ya kuhakikisha mradi huo unatekelezeka kwa wakati ili kuwezesha huduma za mawasiliano zinawafikia wateja wengi zaidi.
Shirika linaendelea na ujenzi mradi huu kwa kasi kubwa kwakushirikiana na Wakandarasi ili kuukamilisha kwa wakati uliopangwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
TTCL inatekeleza mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 32 nchini ambao utasaidia katika kufikisha Mawasiliano ya intaneti kwa wananchi kwa urahisi jambo litakalochangia ukuaji wa matumizi ya TEHAMA katika maeneo mbalimbali.
Kukakamilika kwa mradi huu kutasaidia kuongeza wigo wa mawasiliano, kupunguza gharama za mawasiliano pamoja na kuongeza maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia.
Mradi huu utaongeza uwezo wa biashara na huduma za kifedha, ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa wilaya hizo na kuongezeka kwa upatikanaji wa fursa za ajira.
Ni matarajio ya Shirika kuwa kukamilika kwa mradi huu kutakuwa chachu katika maendeleo ya upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na huduma za afya na elimu kwa kuwezesha upatikanaji wa habari muhimu na mawasiliano kwa wananchi.
Kwa kuzingatia umuhimu huu, upanuzi wa mkongo wa mawasiliano katika wilaya 32 Tanzania unaweza kuwa hatua muhimu katika kukuza maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya watu katika eneo hilo.