TTCL YAZIDI KUJIKITA KIMATAIFA KIBIASHARA
Imeelezwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira thabiti ya kusimamia sekta ya mawasiliano nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kukuza matumizi ya TEHAMA na huduma za kidijitali, na kufungua fursa kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC kutumia miundombinu ya mawasiliano ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye wakati akizungumza katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa kuongeza huduma ya kuwapatia huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa miaka 5 zaidi.
Amesema kujiunga kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano NICTBB ni jambo la kutia moyo na inaonesha nchi hizo zina imani na Tanzania na ndiyo maana hazioni mashaka kushiriana katika kukuza uchumi wa kidigitali katika ukanda wa Afrika Mashiriki.
Alisema uhusiano kati ya Tanzania kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania na Burundi kupitia Burundi Backbone System ulianza mwaka 2019 wakati walipoingia mkataba wa kwanza wa kuwapa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliohusisha kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Burundi-Burundi Backbone System kupitia eneo la Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera na Manyovu upande wa Kigoma.
Ufanisi wa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umepelekea Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kuboresha mawasiliano kati ya nchi hizi mbili.
“Kama Taifa tunajivunia sana mchango wetu katika kuboresha mawasiliano katika Afrika Mashariki. Tunaamini mkataba huu mpya utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania na Burundi kwa kuimarisha uchumi, biashara, na ushirikiano wa kijamii”. Alisema Waziri Nape
Katika hatua nyingine Waziri Nape alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo ya nchi.
Alisema malengo ya serikali ni kuhakikisha mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ifikapo 2025 uwe umefikia kilometa 15,000 na kuunganisha Mikoa na Wilaya zote nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2025.
Alisema upanuzi wa Mkongo wa Taifa ni mojawapo ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ambapo ni matarajio kwamba mradi huo utaleta ufanisi na faida kwa wananchi ikiwa pamoja na kuimarisha uchumi, kuboresha huduma za kijamii, kuunganisha jamii, na kuongeza ushindani wa Kimataifa.
Amebainisha kuwa miradi hiyo inayotekelezwa na serikali ni pamoja na. Awamu ya Kwanza wenye kilometa 4,442 ambayo itafikia wilaya 22 kupitia mradi wa upanuzi wa Mkongo wa mwaka 2021/22 II. Awamu ya Pili wenye kilomita 1,520 ambayo itafikia wilaya 32 kupitia mradi wa upanuzi wa Mkongo na Upanuzi wa Njia Kuu kutoka 800Gbps hadi 2Tbps kwa mizunguko ya Kaskazini na Magharibi kupitia mradi wa 2022/23 III.
Alisema Awamu ya Tatu; yenye kilomita 928 ambayo itafikia Wilaya 5 unajengwa pamoja na upanuzi wa hadi 2Tbps kwenye mradi wa upanuzi wa ndani kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema kusainiwa kwa Mkataba kati ya TTCL na BBS ni fursa na wito kwa nchi zingine za Afrika kujiunga na mkongo wa mawasiliano (NICTBB) ili bara zima la Afrika liunganishwe na mkongo huo hali itakayowezesha kukuza uchumi kwa pamoja.
Aidha Waziri Nape ametoa rai kwa TTCL kuhakikisha BBS wanapata huduma bora na yenye uhakika kama ilivyoainishwa katika Mkataba kutokana na ukweli kuwa BBS inategemea sana huduma za TTCL ili kuendesha shughuli zake kwa ufanisi kibiashara na kujenga uchumi.
Naye Mhandisi Peter Ulanga Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania alisema shirika hilo limekubali kuongeza mkataba na BBS baada ya matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa, kwa Serikali ya Burundi kupitia Burundi Backbone System na kwamba shirika hilo liko tayari kutoa huduma bora kwakuzingatia masharti ya mkataba ili kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Tanzania na Burundi.
“Tunafurahi sana kuona Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ukiendelea kutumika kwa mafanikio katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Ubora wa huduma na gharama nafuu za mkongo huu vimetupa motisha ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu yake ili iweze kuleta tija zaidi na kuchochea shughuli za maendeleo katika nchi zetu za Afrika,” alisema Mhandisi Peter Ulanga
Alisema mapema mwaka jana 2023, shirika lilifanikiwa kusaini Mkataba wa kibiashara wa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Tanzania na Mkongo wa Taifa wa Uganda kwa kushirikiana na Mamlaka ya Taifa ya Teknolojia ya Habari ya Uganda (NITA-U). na kwamba limeishafanikiwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Tanzania na Mkongo wa Taifa wa Malawi kupitia Shirika la Umeme la Malawi (ESCOM).
Aliongeza kuwa hadi sasa, TTCL imefanikiwa kuunganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, na Zambia na kwamba Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeishafika Mtambaswala katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, na juhudi za dhati zinaendelea za kuunganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano utekelezaji wake unaendelea.
Alisema TTCL imeendelea kusimamia na kuendesha miundombinu hii kwa weledi ili iweze kuendelea kuleta manufaa kwa Tanzania na pamoja na nchi jirani ambapo NICTBB imeunganishwa kwenye mikongo ya baharini (submarine cables) kama vile SEACOM, EASSY na sasa Shirika hilo (TTCL) litajiunga na Africa, na kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha mawasiliano Kimataifa.