TTCL YAIMARISHA MAUZO YA FTTH MBEZI 1 KUPITIA PROGRAMU MAALUMU UBUNGO MSEWE
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limefanikiwa kutekeleza programu maalumu ya mauzo ya huduma ya intaneti ya kasi (FTTH) katika eneo la Ubungo Msewe, chini ya mradi wa Mbezi 1, iliyofanyika kwa siku mbili mfululizo, Jumamosi na Jumapili.
Zoezi hilo liliongozwa na Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam Kasikazini, Bw. Aron Msonga, kwa kushirikiana na Watumishi wote kutoka katika mkoa wake wa kibiashara.
Programu hiyo ilikuwa na malengo makuu matatu, ambayo ni kupata wateja wapya wasiopungua 300, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma ya faiba (FTTH) pamoja na kufanya mauzo ya moja kwa moja kwa wateja wa majumbani na biashara.
Katika utekelezaji wa zoezi hilo, timu ya TTCL Mkoa wa Kaskazini, iliwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya Ubungo Msewe, ambapo walipewa elimu juu ya faida za kutumia intaneti ya faiba ikiwemo kasi kubwa, uhakika wa huduma, usalama wa mawasiliano pamoja na mchango wa huduma hiyo katika kuendeleza shughuli za kiuchumi, elimu mtandao na kazi za mbali.
Aidha program hii iliwapa wananchi fursa ya kuuliza maswali na kufanya maombi kwenye mfumo na mara moja kupata huduma hiyo.