
TTCL YAFUTURISHA WATOTO YATIMA NA WAZEE ZANZIBAR
Shirika la Mawasiliano Tanzania –TTCL Corporate Machi 26 mwaka huu limetoa futari kwa Watoto Yatima katika Kituo cha Mazizini na Wazee wa Kituo cha Sebuleni, Zanzibar, lengo likiwa ni kuonesha moyo wa kujali na kusaidia jamii, hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa TTCL Zanzibar, Bw. Hilaly Mwinyi, alisema kuwa Mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kukuza uhusiano na jamii na kwamba shirika linawatambua Watoto Yatima na Wazee kama hazina ya Taifa huku akieleza Wazee ni chanzo cha hekima na heshima katika maisha ya kila siku.
Bw. Mwinvi pamoja na mambo mengine aliwashukuru Viongozi wa Dini na Serikali, kwa kushiriki na kuunga mkono hafla hiyo ambapo shirika linaendelea kuhakikisha pamoja na kuwahudumia wananchi kupitia mawasiliano thabiti linatekeleza pia jukumu la kuisaidia jamii katika nyanja mbalimbali.
Alisema TTCL limefanya hafla hiyo kuonesha kuwa si tu shirika la mawasiliano bali pia chombo cha kuleta furaha na faraja kwa wananchi wenye mahitaji mbalimbali na kwamba futari hiyo ni njia ya kudumisha na kuimarisha mahusiano na jamii.
Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, alilishukuru Shirika hilo kwa kuandaa futari na kutoa zawadi mbalimbali kwa Watoto Yatima na Wazee.
"Michango yenu ya leo inadhihirisha jinsi TTCL ilivyo karibu na jamii na kuwasaidia wanao hitaji," alisema Sheikh Wadi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee, Bw. Hassan Ibrahim Suleiman, alisema TTCL imekuwa mstari wa mbele katika kuihudumia jamii ya watu wenye uhitaji na kwamba ni mfano bora kwa mashirika na taasisi mbalimbali hapa nchini.
"Hii siyo mara ya kwanza kwa TTCL kutuonesha wema, mmekuwa mkifanya haya katika maeneo mbalimbali na mmekuwa mfano kwa mashirika na taasisi zingine," alisema.
Tukio hili liliwashirikisha Wateja na Wadau mbalimbali wa TTCL ikiwa ni ishara ya uthabiti wa uhusiano kati ya shirika na jamii ambapo shirika limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kujihusisha na shughuli za kijamii, ikiwemo kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.