info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL MDHAMINI MKUU HUDUMA ZA MAWASILIANO KIKAO KAZI CHA MSAJILI WA HAZINA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), CPA Moremi Andrea Marwa anashiriki kikao Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma ambacho kinafanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa- AICC Arusha.
Mbali na ushiriki wa Shirika katika kikao hiki, TTCL pia ni Mdhamini Mkuu wa huduma za mawasiliano kupitia huduma ya  *"Public WiFi"  ambayo inatolewa katika maeneo yote ya mkutano kwa kiwango cha gigabit 10 (10Gbps). 

Udhamini huu  unalenga kuhakikisha kikao hicho kinafanyika bila changamoto huku washiriki wakipata fursa ya kutumia mtandao wa kuaminika kwa ajili ya mawasiliano na uwasilishwaji wa taarifa za kikao hicho.
Aidha utekelezaji wa huduma hii ya Intaneti, ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Shirika katika kuhakikisha maeneo yote muhimu ya Umma  na yale ya kimkakati yanawezeshwa na huduma za intaneti yenye kasi kwa matumizi ya wananchi wote. 

Shirika tayari limetekeleza mradi wa interneti ya Umma "Public WiFi"  katika vyuo vya IFM, IAA, SUA, UDSM-CoICT, vituo vya SGR na Mlima kilimanjaro katika vituo vyote mpaka kilele cha mlima huo. 

Mradi huu pia utahusisha  sehemu mbalimbali kama Kumbi za Mikutano, Stendi za Mabasi, Masoko  na sehemu mbalimbali za umma za mapumziko.

Shirika la Mawasiliano Tanzania pia linawakaribisha Washiriki wote kutembelea Banda la Maonesho la shirika lililopo katika Viwanja vya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano- AICC Arusha, ambapo washiriki watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu huduma mbalimbali za mawasiliano, kupata taarifa kuhusu miradi inayotekelezwa, na kuzungumza moja kwa moja na Maafisa Mauzo  juu ya mipango ya kibiashara ya shirika.