info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL KUBORESHA UTOAJI HUDUMA KWA WATEJA

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuboresha huduma zake kwa wateja kupitia teknolojia za kisasa na ubunifu wa huduma, huku likizingatia mahitaji yanayobadilika ya wateja na mazingira ya soko la mawasiliano.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Shirika hilo Bi. Wendelin Mbaga wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja uliofanyika katika Makao Makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Katika maadhimisho hayo Bi. Mbaga alisema Shirika hilo litaendelea kuboresha huduma zake kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuwahudumia wateja wake kwa wakati na kukidhi matarajio yao.

Bi. Mbaga alisisitiza umuhimu wa huduma bora kwa wateja kama njia mojawapo ya kujenga uhusiano mzuri kati ya Shirika na wateja wake na kwamba ni fursa uhimu ya kusikiliza mawazo na maoni ya wateja ili kuboresha huduma wanazozitoa. 

“Tunajivunia kuendelea kutoa huduma bora, na tutaendelea kufanya maboresho zaidi kwa kutumia teknolojia za kisasa, kuboresha miundombinu, na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wetu ili kuwahudumia wateja kwa ufanisi zaidi," alisema Bi. Mbaga

Aidha Bi. Mbaga aliwashukuru watoa huduma kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja ili kuhakikisha changamoto za wateja zinatatuliwa kwa wakati hali itakayosaidia kuboresha uhusiano na kuliendeleza shirika hilo muhimu la mawasiliano nchini. 

Maadhimisho haya aliyoanza Oktoba 7 mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu ya “Above and Beyond” kauli mbiu ambayo inawataka watoa huduma kuwahudumia wateja wao kwa ubora, haraka na ufanisi wa hali ya juu ili kufikia matarajio ya wateja wao kutokana na huduma wanazozitoa.

Kauli mbiu hii inaakisi umuhimu mkubwa wa wateja katika kila hatua ya mafanikio ya biashara au taasisi yoyote kwani inasisitiza kuwajibika kwa wateja wao kwani bila wateja, hakuna kampuni, taasisi au biashara inayoweza kufanikiwa hivyo ni muhimu kuwathamini, kuwahudumia kwa ubora, na kuwaweka wateja katikati ya kila uamuzi wa biashara.

Kutokana na hali hiyo Bi. Mbaga  alisema ni muhimu sana watoa huduma kuwazingatia wateja katika kila hatua ya maendeleo ya shirika hilo kwani wateja wanatoa mrejesho wa moja kwa moja juu ya bidhaa na huduma zinazotolewa ambapo maoni yao yakipewa kipaumbele ni wazi ustawi wa biashara utaimarika.

Wiki ya Huduma kwa Wateja ni Siku Tano za kazi za Wiki ya Kwanza ya Mwezi wa Kumi kila Mwaka ambapo mara nyingi hutarajiwa kuanza kila Tarehe 2 ya mwezi wa kumi. Kwa mwaka huu kutokana na mabadiliko ya kalenda maadhimisho haya yalianza Oktoba 7 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 11 mwaka huu 2024.

Kauli mbiu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu 2024 inatoa fundisho kuwa huduma bora kwa wateja si chaguo tena, bali ni sehemu ya msingi ya mafanikio ya muda mrefu ya biashara yoyote. Watoa huduma wanapaswa kukumbuka kwamba wateja ndiyo moyo wa kila mafanikio, na kuwajali wateja ni msingi wa kujenga uaminifu na ukuaji endelevu.