TANZANIA IMEJIPANGA KUWA KITOVU CHA TEKNOLOJIA NA MAWASILIANO AFRIKA - MARWA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, amepongeza juhudi za Afrika katika kujenga mustakabali wa pamoja wa kidijitali na kuifanya bara hilo kuwa kitovu cha teknolojia, ubunifu, na maendeleo jumuishi, kupitia nguvu ya intaneti ya kasi (broadband) na akili mnemba (AI).
Akizungumza katika Mkutano wa Dunia wa Broadband Association Forum uliofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini Novemba 10 mwaka huu Bw. Marwa alisisitiza kuwa Tanzania iko katika hatua nzuri ya kuongoza mapinduzi ya kidijitali barani Afrika kupitia miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa chini ya dira ya Tanzania ya 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali.
“Broadband na akili bandia si tena hiari, ni injini ya ushindani, ubunifu na ustawi wa bara letu. Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha mawasiliano, biashara mtandao na ubunifu wa kiteknolojia katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini,” alisema Marwa mbele ya washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi 40 duniani.
Katika hotuba yake, Marwa alieleza hatua kubwa zilizofikiwa na Tanzania kupitia Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), ambao umejenga zaidi ya kilomita 14,000 za nyaya za optic faiba, ukiunganisha Mikoa yote, Wilaya na hata nchi jirani ndani ya jumuiya za EAC na SADC.
Alifafanua kuwa NICTBB sasa umeunganishwa na mifumo 11 ya nyaya za baharini za kimataifa, ikiwemo SEACOM, EASSy, 2Africa, na mingine kupitia Dar es Salaam na Mombasa, hatua inayohakikisha huduma zenye ubora wa kimataifa, kasi kubwa na uaminifu wa kiwango cha juu.
“Miundombinu hii imetuwezesha kufikia zaidi ya usajili milioni 99.3 wa mawasiliano na watumiaji milioni 56.3 wa intaneti nchini ambapo mafanikio haya yanayochochea ujumuishaji wa kidijitali na utekelezaji wa huduma muhimu kama Serikali mtandao, mtandao, Kilimo mtandao, Elimu mtandao na mahakama mtandao,” alisema.
Aidha, Bw. Marwa alitaja miradi mipya inayotekelezwa, ikiwemo upanuzi wa Mkongo wa Taifa hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Ziwa Tanganyika hadi Kalemie, ujenzi wa mkongo wa baharini wa Kilimanjaro One Submarine Cable System (KO-SCS) unaounganisha Dar es Salaam na Mauritius, na mradi wa Kituo cha Pan African Green AI & Robotics Data Center ambacho kitakuwa kituo cha kwanza barani Afrika kitakachotumika kwa utafiti na maendeleo ya akili bandia na roboti kwa njia endelevu.
Pia alibainisha mipango ya kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kidijitali na kompyuta nchini, ambacho kitapandisha matumizi ya vifaa vya kisasa kutoka asilimia 36 hadi 100, sambamba na uanzishwaji wa programu ya Wi-Fi bure kwa Umma katika maeneo ya Vyuo Vikuu, Vituo vya Usafiri, Masoko na Hospitali.
Akihitimisha hotuba yake, Marwa aliwaalika wadau wa sekta ya mawasiliano duniani zikiwemo Kampuni za Teknolojia, watoa huduma za intaneti, na wawekezaji ushirikiana na Tanzania katika kujenga bara lenye mtandao wa uhakika, wenye akili bandia, na endelevu.
“Tanzania ipo tayari kuwa daraja la kuunganisha Afrika. Tunakaribisha uwekezaji na ushirikiano ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, kuimarisha ubunifu na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika mapinduzi ya kidijitali,” alisema Marwa.
Mkutano huo wa Kimataifa ulihudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Sekta ya TEHAMA kutoka mabara yote, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Taasisi za fedha, na makampuni ya teknolojia makubwa duniani huku ukisisitiza umuhimu wa broadband na akili mnemba (AI) kama injini ya ukuaji wa uchumi wa Afrika katika zama za kidijitali.