info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

T-PESA YAPAA KIDIJITALI, YAZINDUA AKAUNTI PEPE

Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL ya T-PESA imezindua huduma mpya ya kifedha ya Akaunti Pepe(Virtual Account) ambayo inamuwezesha mtumiaji kufanya miamala ya kifedha kwa usalama na hivyo kuongeza chachu katika kukuza matumizi ya kifedha kidijitali. Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hii Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania -TANTRADE, Bi. Latifah Khamis amesema ujio wa huduma hii ni sahihi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inasisitiza matumizi ya teknolojia ya mawasiliano na TEHAMA katika kujenga Tanzania ya Kidigitali. Amesema matumizi ya mifumo ya Kidigitali hususani matumizi ya fedha mtandao yataleta mageuzi makubwa katika kukuza biashara na uchumi na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi. "..Nchi yetu inahitaji teknolojia zitakazoleta mageuzi makubwa katika ujenzi wa uchumi wa Tafa letu sambamba na kuimarsha biashara" Bi. Latifah. Amesema TANTRADE, imefarijika sana kuona huduma hii kwa kuwa itaenda kugusa eneo la Biashara ambapo huduma hii itarahisisha kupokea malipo na kufanya shughuli za kifedha kwa uhakika sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi Bi. Latifah. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa T-PESA, Bi. Lulu Mkude amesema T-Pesa ni mdau mkubwa katika kukuza matumizi ya mifumo ya kidigitali katika shughuli za kiuchumi na kijamii na dhamira ya kampuni hiyo ni kuhakikisha inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi wa Tanzania ya Kidigitali. "Leo, tunasherehekea ubunifu wa kipekee kabisa kutoka T-PESA wa kufungua akaunti yako kiganjani mwako popote pale ulipo ijulikanayo kama Akaunti Pepe (Virtual Account), hii ni suluhisho la matumizi ya huduma za kifedha ambalo linamwezesha kila mmoja wetu, kufurahia huduma za kifedha kidijitali kupitia ubunifu huu mpya na wakipekee "amesema Bi, Mkude Amesema huduma hii itamwezesha kila mmoja kila mteja kupitia simu janja kuweza kufungua akaunti yake na kupata huduma za kifedha na zenye uhakika. Huduma ya Akaunti Pepe (Virtual Account)ni teknolojia inayoruhusu wateja kutuma na kupokea pesa kwa urahisi, kulipa bili, na kufanya manunuzi kwa njia ya kidijitali pasina kuwa na SIMCARD. Aidha, kupitia Akaunti Pepe mteja anaweza kupata huduma za kifedha zenye uhakika, rahisi na salama, vilevile huduma hii inawezesha kuwa sehemu ya mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya kifedha nchini Tanzania. Miongoni mwa faida za huduma hiyo itasaidia kuongeza wigo wa matumizi ya kifedha kwa watu wasio na akaunti za benki. Mkurugenzi wa T-PESA Bi. Mkude amesema kuwa kufungua huduma hiyo ni rahisi ambapo Mteja atafunga program Rununu ya T-PESA (T-PESA App), baada ya kufungua Mteja ataingiza namba yake ya simu, atapata ujumbe mfupi OTP na kisha ataweka namba yake ya NIDA, kisha ataweka alama ya kidole na kuweka nywila (password) yake na hapo ataona ujumbe unaomuonesha kuwa amefanikiwa kutengeneza akaunti pepe yake ya T-PESA.