
SERIKALI YAZINDUA MAFUNZO YA MRADI MKUBWA WA MAWASILIANO VIJIJINI: TTCL KUJENGA MINARA 621
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezindua rasmi mafunzo ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa usambazaji wa mawasiliano katika maeneo ya vijijini, ambapo Taasisi mbili za Serikali ikiwa ni pamoja na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zimenufaika na mradi huo.
Kupitia mradi huu, TTCL imepewa jukumu la kujenga minara 621 ambayo itatumia teknolojia ya kisasa ya 4G na 2G kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano maeneo ya pembezoni mwa nchi, huku TBC ikikabidhiwa minara 15 kwa ajili ya kuimarisha huduma za utangazaji vijijini.
Mradi huu unaogharimu jumla ya Dola Milioni 128 za Kimarekani, utatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka miwili (2), kwa lengo la kuongeza uwiano wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na taarifa kwa wananchi walioko maeneo yasiyofikika kwa urahisi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa uzinduzi huo, Bi Salome Kossy, ambaye ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala katika wizara hiyo, alisema kuwa mafunzo haya ni sehemu muhimu ya maandalizi ya utekelezaji bora wa mradi huo na kuhakikisha usimamizi na uendeshaji wake unakuwa endelevu hata baada ya kukamilika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francic, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, alitoa shukrani za dhati kwa Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawawezesha watendaji kusimamia kikamilifu miradi hiyo na kuendesha mitambo kwa ufanisi mara baada ya kukamilika.
Aliongeza kuwa, mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya msingi ya kupata taarifa, kuwasiliana, na kuunganishwa na dunia kwa njia ya kidigitali na kwamba kukamilika kwake kunatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hasa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa hayana huduma za mawasiliano ya uhakika.