info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

SERIKALI NA WADAU WA SEKTA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI WAKUTANA JIJINI ARUSHA KUJADILI UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA TAIFA WA UCHUMI WA KIDIGITALI (2024-2034)

Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya Kikao Kazi Maalum na Wadau wa Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari cha kujadili utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali kwa kipindi cha 2024 hadi 2034. 

Kikao hicho kilijikita katika kujadili changamoto, fursa na mikakati ya kuhakikisha Tanzania inatumia teknolojia ya kidigitali kuimarisha uchumi wake na kuongeza tija katika sekta mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa (Mb), alisisitiza kuwa mkakati huu utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano, biashara, elimu na huduma za serikali kwa kutumia mifumo ya kidigitali. 

Alieleza kuwa serikali inawekeza katika miundombinu thabiti, kama vile Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ili kuwezesha upatikanaji wa intaneti ya kasi ili kuwezesha huduma za kidigitali kwa wananchi wote.

Katika kutekeleza mkakati huu, serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, imeanzisha kampeni ya usalama mitandaoni inayoitwa "Sitapeliki", yenye lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna bora ya kujilinda dhidi ya ulaghai wa mtandaoni. 

Waziri Silaa alibainisha kuwa usalama wa mtandao ni jambo la msingi katika kuhakikisha kwamba maendeleo ya kidigitali yanapokelewa kwa ufanisi na wananchi wanaweza kutumia mifumo ya kidigitali kwa uhakika.

Kikao kazi hiki pia kimeangazia pia nafasi ya mashirika ya mawasiliano, hususan TTCL, ambayo ni mdau muhimu katika usimamizi wa miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano. 

TTCL inasimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kituo cha kuhifadhi Data cha Kitaifa (Data Center), ambacho ni mhimili wa huduma za kidigitali nchini ambapo Viongozi wa TTCL walieleza wadau wa kikao hicho kuwa wanashirikiana na serikali kuhakikisha miundombinu hiyo inapanuliwa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusaidia taasisi na biashara kutumia teknolojia ya kisasa.

Aidha, wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano walisisitiza umuhimu wa sera rafiki zinazowezesha ubunifu na maendeleo ya mifumo ya kidigitali na kupendekeza serikali iendelee kuwekeza katika teknolojia ya 5G, kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kidigitali kwa gharama nafuu, na kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanaunganishwa na mtandao wa kasi.

Katika hatua nyingine kikao hicho kimejadili umuhimu wa kuwaandaa vijana kwa uchumi wa kidigitali kwa kuwapa maarifa na ujuzi wa TEHAMA ambapo mpaka sasa serikali imetangaza mpango wa kushirikiana na Vyuo Vikuu na Taasisi za mafunzo kutoa kozi maalum za teknolojia ili kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya taifa inakuwa na ujuzi wa kisasa wa kidigitali ili kuwezesha vijana wengi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali na kujipatia ajira kupitia majukwaa ya kidigitali.

Kikao kazi hicho kilikubaliana kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkakati huu, mfumo huu utahakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati na changamoto zozote zinazojitokeza zinatatuliwa kwa haraka na kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kutosha kuhusu matumizi salama na sahihi ya mifumo ya kidigitali.

.