NAPE ATAMBUA MCHANGO WALIOSHIRIKI UZINDUZI MLIMANI KILIMANJARO.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) awatunuku tuzo na vyeti kwa washiriki 57 walioshiriki katika uzinduzi wa huduma ya mawasiliano Intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Disemba 13, 2022. Jumla ya Washiriki 57 kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Shirika la Mawasiliano Tanzania, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Taasisi za Umma na Binafsi na Vyombo vya habari walishiriki zoezi la kupanda Mlima na washiriki 39 walifanikiwa kufika katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro wakati washiriki wengine waliishia katika Kituo cha Mandara, Horombo, Kibo na Gilman’s. Tuzo hizo zimetolewa katika hafla iliyofanyika Julai 22, mwaka huu Marangu Gate, Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutambua mchango wa wafanyakazi waliofanikisha ujenzi wa mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro na walioshiriki uzinduzi wa huduma hiyo katika kilele cha mlima Kilimanjaro Disemba 13,2022. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Nape amesema safari ya kwenda kuzindua huduma ya mawasiliano ya intaneti kilele cha mlima Kilimanjaro ilianza Desemba 09, 2022 kuanzia kituo cha Marangu Gate, Mandara, Horombo, Kibo, Gilman’s, Stella na Desemba 13, 2022 tulifika Kilele cha Mlima Kilimanjaro Uhuru Peak (5895m) na kufanikisha kuweka historia ya kuzindua huduma ya mawasiliano ya intaneti katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro. “uwepo wa mawasiliano ya Intaneti katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro yatasaidia kukuza sekta ya utalii, sekta ya mawasiliano na kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa watalii kupata huduma za mawasiliano wakiwa katika shughuli za kiutalii, pia Mradi huu pia utasaidia Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika utekelezaji wa mkakati wa kujenga Tanzania ya Kidijitali” amesisitiza Waziri Nape. Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi, Zuhura Sinare Muro amesema matukio makubwa yameanza kuonekana kwenye mlima Kilimanjaro kwa sababu ya uwepo wa huduma ya Intaneti, hivyo “Tunaimani kuwa TTCL itakuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za serikali za kutangaza vivutio vya utalii na sekta ya mawasiliano” amesema Bi. Zuhura Muro. Naye, Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa Shirika limeshaanza ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano ya Intaneti katika njia ya Machame Gate na tunatarajia kukamilika kabla ya mwezi Septemba mwaka huu 2023, kukamilika kwa mradi huu utasaidia kuongezeka upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro.