info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MKURUGENZI MKUU WA WAKALA WA MAENDELEO YA HUDUMA ZA MTANDAO NCHINI COMORO AFANYA ZIARA TTCL

  Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Huduma za Mtandao nchini Comoro (ANADEM) Bw. Said Mouinou afanya ziara ya kikazi Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL leo Novemba 23,2024 kwa lengo la kupata uzoefu wa usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano nchini Tanzania. 

Katika ziara hiyo, wageni kutoka ANADEM wameongozana na Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu pamoja na Viongozi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw.David Mwankenja

Akizungumza wakati akiwakaribisha Wageni hao kutoka nchini Comoro, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania CPA.Moremi Marwa amewashukuru ANADEM kwa kuchagua Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuwa ya kujifunza na kuonesha nia yakushirikiana katika kiumarisha  sekta ya mawasiliano. 

“TTCL tuko tayari kushirikiana na ndugu zetu kutoka Comoro ukizingatia TTCL inauzoefu miaka mingi katika sekta ya mawasiliano, mashirikiano baina ya nchi hizi mbili yataleta tija katika kusukuma maendeleo katika nyakati hizi za ukuaji wa maendeleo ya kidigitali” amesema CPA Marwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ANADEM, Bw. Mouinou  amepongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika kuendesha na kusimamia miundombinu ya mawasiliano ambayo imechangia Tanzania kupiga hatua kwenye maendeleo ya kidigitali. 

“Tumefurahi kujua namna ambavyo Shirika la Mawasiliano Tanzania limekuwa likifanya kazi zake, mmetupitisha katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sehemu za mitambo inayotumika katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kimawasiliano na tumeona tofauti kubwa iliyopo Nchini kwetu na hapa, Tumekuwa katika mpango wa kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika kimawasiliano tunafikiri tutayapata mengi zaidi kupitia uhusiano katika ya Comoro na Tanzania katika Nyanja hiyo” amesema Bw. Mouinou

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu amewataka TTCL na ANADEM kuhakikisha wanashirikiana katika kubadilishana uzoefu na maarifa katika ya sekta ya mawasiliano ili  nchi hizi mbili zinufaike  katika shughuli za maendeleo.

“Tanzania na Comoro ni ndugu na tumekuwa na mashirikiano katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, ni fursa nyingine kwa ANADEM kushirikiana na TTCL katika sekta ya mawasiliano ukizingatia TTCL inauzoefu na wataalam wenye ujuzi katika masuala ya mawasiliano” amesema Mhe.Saidi. 

Wageni hao kutoka ANADEM walipata fursa ya kuzungumza na Menejimenti ya TTCL, kutembelea miundombinu ya mawasiliano ikiwemo Kituo cha Uangalizi na Uendeshaji wa Mtandao (NOMC) pamoja na Kituo cha Taifa cha Kutunza Data Kimtandao-NIDC